Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka wataalam wa ununuzi na ugavi nchini kizingatia misingi ya maadili ya taaluma yao ili kuiwezesha Serikali kuleta maendeleo kwa wananchi wake.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Desemba 17, 2024 wakati
akifungua Kongamano la 15 la Wataalam wa Ununuzi na Ugavi linaloendelea Jijini
Arusha.
Amesema wataalam wa ununuzi na ugavi ni muhimu katika
kuchagiza maendeleo na Serikali inawategemea ili kufanikisha mipango yake.
“Wataalam wa manunuzi na ugavi mna mchango mkubwa, zaidi
ya asilimia 70 ya bajeti nzima ni kwa ajili ya manunuzi, hivyo kuweni
waadilifu, Chukieni Rushwa na kushauri namna bora ya kufanikisha mipango ya
Maendeleo,” amesema Dkt. Biteko.
Amesema kutokana na ukubwa wa majukumu yao kuna uwezekano
rushwa kubwa ikapita mikononi mwao, hivyo majadiliano haya yawawezeshe kuzuia
na kukabiliana na vitendo hivyo.
Aidha, Dkt. Biteko amesema ni wajibu wa wataalam
kujisimamia na kulinda taaluma yao kwa wivu mkubwa ili taaluma hiyo isiingiliwe
na watu wasiokuwa na sifa zinazohitajika huku akizitaka mamlaka husika
kuwatambua na kuwamotisha wataalam wenye sifa kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, Dkt. Biteko amewataka washiriki wa Kongamano
hilo kujifanyia tathimini kuhusu utendaji wao wa kazi ili kuondokana na
Changamoto zinazoweza kuichafua taaluma ya ununuzi na ugavi.
“Zipo sauti nanyi mnazisikia, ili uweze kupata tenda
lazima kuwa na urafiki na Afisa ununuzi, wanasema ukifuata taratibu za ununuzi
gharama zinaongezeka zaidi ya kawaida, wengine wanasema siri za tenda
zinapatikana miongoni mwa watumishi, wengine wanalaumu na wengine wanasifia,
Jambo la msingi sikilizeni sauti za watu na mjitathimini,” amesisitiza
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Chande
amewataka washiriki kufanya kazi zao kwa kushirikiana huku Wizara yake
ikiendelea kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili wataalam wa ununuzi
na ugavi.
Amesema miongoni mwa mambo yanayosababisha mkwamo
Serikalini ni pamoja na Wivu, choyo na fitna miongoni mwa watumishi, hivyo
amewataka kuondokana na mambo hayo ili kukua na kujiletea maendeleo.
“Sheria ya ununuzi wa umma sura 410 inawalinda wataalam
wa ununuzi na ugavi hivyo watembee kifua mbele na kuhakikisha wanafanya kazi
kwa mujibu wa sheria zilizopo”.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na
Ugavi (PSPTB) Benezeth Ruta ameishukuru Serikali kwa kutenga fedha
zinazoiwezesha taaluma hiyo kusonga mbele.
Amesema Bodi hiyo inaendelea na utekelezaji wa Sheria Na.
23 ya mwaka 2007 kuhakikisha kuhakikisha Wataalam wanaofanya shughuli za
ununuzi na ugavi wana sifa stahiki za kufanya kazi hizo.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni