Wasiojulikana wadaiwa kumteka Abdul Nondo

 

Chama cha ACT Wazalendo kimedai kuwa Mwenyekiti wake wa Ngome ya Vijana Abdul Nondo ametekwa leo asubuhi na watu wasiojulikana alipowasili Jijini Dar es Salaam akitokea mkoani Kigoma.

Nondo alikuwa sehemu ya viongozi wa kitaifa wa chama hicho walioongoza kampeni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwenye mikoa ya magharibi mwa Tanzania.

Taarifa iliyotolewa leo na Naibu Katibu wa Haki za Binadamu na Vyombo vya Uwakilishi wa Wananchi ACT Wazalendo Mbarala Maharagande imesema Nondo aliwasili stendi Magufuli iliyopo Mbezi kwa usafiri wa basi la Saratoga lenye namba za usajili T 221 DKB.

Taarifa hiyo imesema mashuhuda wa tukio hilo wamedai kulikuwa na purukushani katika utekaji wa Nondo hali iliyosababisha begi lake dogo la nguo na pingu iliyobebwa na mmoja wa watekaji kudondoka.

Chama cha ACT Wazalendo kimelitaka Jeshi la Polisi kufuatilia tukio hilo ili kufanikisha kupatikana kwa Nondo anapatikana akiwa salama.



Chapisha Maoni

0 Maoni