WAZIRI MKUU,
Mhe. Kassim Majaliwa amesema kuwa uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na
China umeendelea kukua ambapo mwaka 2023 biashara kati ya nchi hizo ilifikia
dola bilioni 8.78.
Amesema kuwa
ukuaji na ushirikiano huo wa makampuni ya China na wafanyabiashara wa Tanzania
umeleta maendeleo katika ukuaji wa viwanda vya ndani, kutengeneza ajira, ujenzi
wa miundombinu na uboreshaji wa hali ya maisha ya Watanzania.
Amesema hayo
leo (Novemba 30, 2024) wakati wa hafla ya Kumbukumbu ya Miaka Kumi ya Jumuiya
ya Kukuza Ushirikiano kati ya China na Tanzania, iliyofanyika katika ukumbi wa
mikutano wa Chuo Kikuu cha Dar ea Salaam, Jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa
Kampuni za China zimezindua takribani miradi 1,274 ambayo kwa kiasi kikubwa
pamoja na mambo mengine, imezalisha ajira kwa Watanzania. “Huu ni uthibitisho
wa jinsi ushirikiano wetu unavyolenga kutoa fursa kwa wananchi wetu.”
“Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anathamini mchango wa
China katika maendeleo ya Tanzania kwenye sekta mbalimbali zikiwemo za
biashara, miundombinu na utamaduni,” amesema Mhe. Majaliwa.
Aidha
amesema kuwa China ni moja ya mshirika mkubwa wa kibiashara na uwekezaji kwa Tanzania
na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo kwenye sekta za kilimo, madini,
viwanda na maendeleo ya miundombinu.
Ameongeza
kuwa China imekuwa mshirika muhimu katika kuisaidia Tanzania kukabiliana na
majanga ya kiafya ikiwemo magonjwa ya kuambukiza na changamoto za afya ya mama
na mtoto. “China imekuwa ikitoa timu za wataalam, kuchangia vifaa, na kusaidia
kujenga miundombinu ya afya. Ushirikiano huu umeokoa maisha ya wengi na
umehakikisha kwamba watu wetu wanapata huduma bora za matibabu.”
Akizungumza
kuhusu Jumuiya ya Kukuza Urafiki kati ya Tanzania na China, Mheshimiwa Majaliwa
amesema jumuiya hiyo imekuwa mchango mkubwa katika kukuza na kuendeleza
uhusiano kati ya mataifa hayo mawili ikiwemo kuwaleta watu pamoja, si tu kutoka
kwa serikali, bali kutoka nyanja mbalimbali za maisha.
0 Maoni