Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa wanachama wa CEO Roundtable of Tanzania (CEOrt) kuvumbua njia zinazotekelezeka katika kuhamisha teknolojia zitakazowasaidia vijana ambao ni idadi kubwa ya Watanzania kwa sasa.
Kwa mujibu
wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Mpango amesema hayo
jana jioni Novemba 30, 2024 alipomwakilisha Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan
katika sherehe ya kufunga mwaka ya CEOrt iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Amesema ni
muhimu kuwasaidia vijana katika teknolojia za kijani, kuunga mkono katika
tafiti na maendeleo pamoja na kuanzisha vituo atamizi vya teknolojia.
Dkt. Mpango
amewasihi kupitia upya vigezo vya kujiunga na CEOrt ili kuongeza idadi ya
vijana kutoka biashara zinazochipukia kama vile katika sekta ya Burudani,
Tehama na Michezo.
Awali,
Mkurugenzi Mtendaji wa CEOrt, Santina Benson amesema jukwaa hilo linajivunia
hatua mbalimbali za maendeleo ikiwamo kuitisha majukwa ya kujadili maendeleo ya
kiuchumi, kupitia sekta za viwanda na biashara.
CEO
Roundtable of Tanzania inajumuisha Wakurugenzi na Watendaji Wakuu kutoka
Makampuni zaidi ya 200 kutoka sekta mbalimbali nchini ambapo wanachama wake
wanachangia katika maeneo ya kukuza na kuendeleza uchumi ikiwemo uchangiaji wa
kodi na kuimarisha uongozi nchini kupitia programu za mafunzo.

0 Maoni