Leo Tanzania
imeandika historia nyingine katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya umeme baada
ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko kuzindua
utekelezaji wa mradi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 400 kutoka
Chalinze hadi Dodoma na upanuzi wa vituo vya kupoza umeme vya
kilovoti 400 Chalinze-Pwani na Zuzu-Dodoma.
Mradu huo wa
umeme uliozinduliwa utawezesha umeme wote unaozalishwa katika mradi wa
kuzalisha umeme wa JNHPP kufika katika maeneo yote ya mikoa iliyopo Kanda ya
Kaskazini, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kati, Kanda
ya Magharibi, Migodi, Viwanda na kuimarisha biashara ya umeme Mashariki na
Kusini mwa Afrika.
Dkt. Biteko
amesema kutekelezwa kwa mradi huo
kunatokana na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuendelea kutoa fedha za
kutekeleza miradi mbalimbali pamoja na miongozo yake ya namna bora ya
kutekeleza miradi ili kuhakikisha nchi inakuwa na umeme wa uhakika kwa lengo la
kukidhi mahitaji ambayo yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku kutokana na ukuaji
wa shughuli za kiuchumi na kijamii.
Amesema kuwa
kutokana na jitihada hizo zinazofanywa na Rais Samia katika kuendeleza miradi
ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme imepelekea Tanzania kuwa kinara
barani Afrika katika usambazaji wa umeme kwa wananchi na hii ni kutokana na
takwimu zilizotolewa na Benki ya Dunia.
Ameeleza kuwa,
Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea na jitihada za kuimarisha upatikanaji wa
nishati ya umeme nchini ambazo zimewezesha kuongeza uwezo wa mitambo ya kufua
umeme iliyopo nchini hadi kufikia Megawati 3,169.26 ambapo mahitaji ya juu ya
umeme nchini kwa sasa yamefikia Megawati 1,888.72 ambapo mahitaji hayo
hayajawahi kufikiwa kutoka nchi ipate Uhuru na hii ikimaanisha kuwa uchumi
unazidi kukua kutokana na kuongezeka kwa shughuli za maedeleo.
“Kuimarika
kwa uzalishaji wa umeme nchini kumechangiwa na kuanza uzalishaji katika
Mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) wenye uwezo wa kuzalisha
Megawati 2,115 ambao hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 99.6 na jumla
ya Megawati 1,175 za umeme zinazalishwa na kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa,” amesema
Dkt. Biteko.
Katika Hafla
hiyo, Dkt. Biteko amekemea vikali wahujumu wa miundombinu ya umeme ambao
amesema kuwa wanarudisha nyuma uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika
kuwafikishia wananchi nishati ya uhakika na kuagiza Vyombo vya Ulinzi na
Usalama kuchukua hatua kali kwa wahujumu hao ambao oia wamekuwa wakikosesha
wananchi umeme pale miyndombinu inapoharibiwa.
Kuhusu
Wakandarasi wa mradi huo, Kampuni ya TBEA kutoka China, amewataka wahakikishe
mradi unakamilika kwa wakati ili wananchi wapate manufaa yaliyokusudiwa
ikiwa pia ni maelekezo ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Dkt. Biteko
ametumia hafla hiyo kuwakumbusha viongozi na wananchi kuhusu jitihada za
Serikali katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kutimiza
lengo la Serikali la asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya
kupikia ifikapo mwaka 2034.
Katika
muendelezo wa jitihada hizo, amesema Serikali imetoa ruzuku kwa mitungi ya gesi
zaidi ya 400,000 itakayouzwa kwa nusu gharama ya bei ya soko ambapo mitungi
hiyo inasambazwa katika Mikoa yote Tanzania Bara.
Ametoa wito
kwa Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia kwa kutumia majiko ya gesi na
teknolojia mbalimbali kulingana na mazingira ikiwemo nishati ya umeme kwani
nishati hizi ni miongoni mwa nishati safi, salama na ya gharama nafuu
ikilinganishwa na matumizi ya kuni na mkaa.
Vilevile
ametoa wito kwa wadau mbalimbali na wafanyabiashara nchini kuhakikisha majiko
yanayotumia nishati fanisi ya umeme yanapatikana kwa wingi na kwa bei nafuu ili
wananchi wengi katika maeneo mbalimbali wakiwemo wa vijijini waweze kutumia
umeme kwa ajili ya kupikia.
Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Innocent Bashungwa ameipongeza Wizara ya Nishati
na TANESCO kwa uzinduzi wa mradi huo wa
usafirishaji umeme na upanuzi wa vituo vya kupoza umeme vya Zuzu Dodoma
na Chalinze na kueleza kuwa utekelezaji wa mradi huo unaakisi dhamira ya Rais
Dkt. Samia ya kutaka watanzania wapate nishati ya uhakika.
Bashungwa
amesema kuwa Serikali inatoa fedha nyingi ili kutekeleza miundombinu ya umeme
hivyo Wizara yake itahakikisha miundombinu hiyo inalindwa kwa wivu mkubwa na
kuwashughulikia wahalifu wa moundombinu hiyo.
Kwa uoande
wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amempongeza Rais, Dkt.Samia Suluhu
Hassan kwa uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanyika katika Sekta ya Nishati na
pia amempongeza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt.Doto Biteko kwa
kusimamia Sekta kwa weledi, ufanisi, uzalendo na uchapakazi wa hali ya juu.
Amesema
mradi uliozinduliwa leo ni muhimu kwani Tanzania inategemewa kuimarisha hali ya
umeme kwa nchi za Mashariki mwa Afrika kupitia miradi ya uzalishaji na
usafirishaji umeme ambayo inaendelea kufanyika.
Amesema moja
ya masuala yaliyokuwa yakitiliwa mkazo katika
Mkutano uliohusu biashara ya kuuziana umeme na kununua umeme kwa nchi
Wanchama Mashariki mwa Afrika (EAPP) ni uunganishaji umeme kati ya Tanzania na
Kenya ambapo leo laini hiyo ya umeme ya kV 400 imewashwa na
pongezi zimetolewa kwa Rais Samia na Dkt. Biteko kwa kutekeleza mradi huo.
Kwa upande
wake, Katibu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema sasa nchi
inazalisha zaidi ya megawati 3000 za umeme na hii inaifanya Tanzania kuwa nchi
inayozalisha umeme mwingi kuliko nchi zote za Afrika Mashariki na hivyo kutoa
fursa kwa Tanzania kufanya biashara ya umeme na nchi nyingine za Afrika iikwemo
Burundi, Rwanda, Uganda na Kenya.
Amesema
mradi huu utaenda katika kanda mbalimbali ikiwemo mikoa ya Kaskazini na kuingia
hadi nchini Kenya.
Awali
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga alisema mradi wa
kusafirisha umeme kutoka Chalinze hadi Dodoma umegawanyika katika sehemu kuu
mbili ambazo ni ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme katika msongo wa
kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma yenye urefu wa kilomita 345 na upanuzi
wa vituo vya kupokea na kupoza Umeme vya Chalinze (400/220/132kV) mkoani Pwani
na Zuzu (400/220/33kV) Mkoani Dodoma.
Alisema malengo
ya mradi huo ni kuwezesha usafirishaji wa umeme wote (2,115MW) utakaozalishwa
katika Bwawa la JNHPP na kuufikisha kwenye maeneo yote ya mahitaji ya umeme,
hatua itakayosaidia kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme kwenye Gridi ya
Taifa na kuongeza uwezo wa kusafirisha umeme kwenda mikoa yenye viwanda na
migodi ya uchimbaji madini ya Kaskazini Magharibi, Kaskazini Mashariki, Kanda
ya Kati na Kusini mwa Tanzania.
Alieleza
kuwa, lengo lingine la mradi ni kuwezesha zoezi la uunganishaji umeme kwa
pamoja katika mifumo ya Mashariki mwa Afrika (Eastern Africa Power Pool - EAPP)
na Kusini mwa Afrika (Southern Africa Power Pool - SAPP) na hivyo kuwezesha
kufanyika kwa biashara ya nishati ya umeme kikanda (Regional Power Trading).
Aliongeza
kuwa, Mradi husika unagharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100 kwa
jumla ya gharama ya Shilingi 513 Bilioni ambapo Mkandarasi Kampuni ya TBEA
kutoka China ameshalipwa malipo ya awali ya kiasi cha Shilingi bilioni
107.93 ambayo ni asilimia 20 ya gharama za mradi.
Alieleza
kuwa katika mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme, kazi mbalimbali
zimeanza na mradi utakamilika mwaka 2026 mwezi Septemba huku mradi wa upanuzi
wa vituo vya kupoza umeme kazi pia zinaendelea na mradi utakamilika Septemba
2026.
Mkuu wa Mkoa
wa Pwani, Abubakari Kunenge amesema mradi huo ni uthibitisho wa kazi kubwa na
nzuri za Dkt. Samia Suluhu Hassan na kwamba umeme huo utafaidisja Tanzania na
nchi nyingine za Afrika na ni sehemu pia ya uhamasishaji wa nishati safi ya
kupikia kwani wananchi watatumia umeme huo kupikia.
Mkuu wa Mkoa
wa Morogoro, Adam Malima amesema wananchi mkoani Morogoro wanatambua kazi
kubwa iliyofanywa na Rais Samia katika kuendeleza miradi ya umeme ikiwemo
kukamilisha miradi ya miaka mingi ukiwemo wa kuunganisha umeme kati ya Tanzania
na Kenya.
Mwakilishi
wa Wadau wa Maendeleo katika hafla hiyo, Wendy Hughes ambaye ni Mkurugenzi wa
Benki ya Dunia Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika ameipongeza
Serikali ya Tanzania kwa kujikita katika kuiimarisha gridi ya taifa ya umeme
ambayo ni muhimu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii pamoja na kutoa uhakika
wa usalama wa nishati.
Amesema
kuwapo kwa mifumo imara ya usafirishaji umeme itafanya wananchi kufikishiwa
umeme wa uhakika katika maeneo mbalimbali ya nchi na pia ni sehemu
ya utekelezaji wa mpango wa kufikisha umeme kwa watu milioni 300 barani Afrika
ifikapo 2030.
Ameahidi
kuwa Wadau wa Maendeleo wataendelea kutoa ushirikiano kwa Tanzania ili
kukamilisha mipango mbalimbali ya maendeleo ambayo nchi imejiwekea.
0 Maoni