Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaahidi kuendelea kushirikiana na Umoja wa
Ulaya (EU) katika kufanya utafiti wa kina utakaosaidia kupata taarifa sahihi za
maeneo madini yanapopatikana ili kuongeza uwekezaji katika uvunaji rasilimali
madini hususani madini mkakati kwa manufaa na maslahi ya Watanzania.
Hayo
yamesemwa leo Desemba 11 Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Madini, Mheshimiwa
Anthony Mavunde alipokutana na ujumbe wa uwakilishi kutoka EU ukiongozwa na Bw.
Hanspaul Stausboll- ambaye ni Mkurugenzi wa Miradi ya EU Bara la Afrika Kusini
mwa Jangwa la Sahara.
“Utafiti ni
moyo wa sekta ya madini, na ndiyo maana Serikali ya Awamu ya Sita chini ya
uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka kipaumbele katika
utafiti wa kina wa madini kupitia mkakati kabambe ujulikanao kama Vision 2030
ambao umelenga kuongeza eneo la utafiti kutoka asilimia 16 ya sasa mpaka
asilimia 50 ifikapo mwaka 2030. Ni dhahiri kazi hii ni kubwa na Serikali
haiwezi kuifanya peke yake pasipo wadau."
"Taarifa
njema ni kwamba tayari Serikali tumeshaanza kufanya kazi na EU katika utafiti
kupitia Ubalozi wa Hispania nchini. Yapo maeneo ambayo tumeyatambua kwa ajili
ya mradi wa kufanya utafiti wa kina wa kurusha ndege na tupo katika hatua za
mwisho za kuanza kwa mradi huo wenye manufaa makubwa kwa Nchi yetu,” aliongeza
Waziri Mavunde.
Aidha,
Waziri Mavunde alibainisha kwamba mazungumzo hayo na ujumbe wa EU yamejikita
katika kuimarisha mashirikiano kwenye uendelezaji sekta ya madini huku
ikichagizwa na ukweli kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi chache ulimwenguni
zilizobarikiwa madini mbalimbali yakiwemo ya kimkakati kama graphite ambayo ni
kivutio kwa wawekezaji wengi kutokana na mwelekeo wa dunia katika kupunguza
hewa ukaa ifikapo 2050 kwa matumizi ya nishati safi.
“Eneo la
pili tulilozungumza ni eneo la kuyaongezea thamani madini yetu ndani ya nchi
badala ya kusafirisha yakiwa ghafi ambapo Nchi tunapoteza mapato, ajira na
ustawi wa watanzania. Haya ndio maagizo
ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kutaka viwanda vya kuongeza thamani
madini kujengwa nchini, hili pia limesisitizwa na Sera yetu ya madini,”
alisisitiza Mhe. Mavunde.
Amesema,
miradi mbalimba inaendelea kufanyika nchini ikiwemo mradi mkubwa unaojengwa
Ngara, mkoani Kagera wa Nikel ikihusisha Kampuni ya Tembo Nickel ambayo
Serikali ni mbia. Kupitia mradi huo wa Nikeli ambapo Kampuni kubwa ya BHP
anaingia kama mwekezaji, kinakwenda kujengwa kiwanda kikubwa cha usafishaji wa
madini ya metali pale Kahama kwenye eneo la Buzwagi Special Economic Zone
ambacho kitakuwa na thamani ya zaidi ya Dola Milioni 500.
Vilevile,
Waziri Mavunde alieleza fursa iliyopo katika mradi wa vijana na wanawake kwenye
sekta ya madini ujulikanao kama Mining for Brighter Tommorow (MBT) na kutoa rai
kwa EU kutoa ushirikiano zaidi katika programu hiyo ili iweze kuleta tija
katika kufikia uchumi wa kati wa juu na kuongeza pato la Mtanzania mara mbili
ya ilivyo sasa ifikapo kama malengo ya Dira ya Maendeleo 2050 ilivyoeleza.
Naye
Mkurugenzi wa Miradi wa EU kwa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Bw. Hanspaul
Stausboll alionesha kufurahishwa na hatua ambazo Serikali inazichukua katika
uendelezaji wa sekta ya madini na kusisitiza kwamba EU ipo tayari kushirikiana
na Tanzania katika kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kipaumbele
ikiwemo utafiti, ujenzi wa miundombinu katika maeneo ya migodi na mafunzo kwa
vitendo ili kuongeza ujuzi kwa Watanzania.
0 Maoni