Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema
malengo makuu ya Rasimu ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ni kugusa moja kwa moja katika kuboresha
maisha ya watu, elimu, afya, ustawi wa amani na haki pamoja na kuwa na Dira
jumuishi ambayo itamshirikisha kila mwananchi kutoa mchango wake kwa maendeleo
ya Taifa.
Rais Dk.
Mwinyi ameyasema hayo alipozindua rasimu ya
kwanza ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hoteli ya Golden Tulip Uwanja
wa ndege Mkoa wa Mjini Magharibi, hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali
wa Serikali za SMT na SMZ akiwemo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Kassim Majaliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman
Abdulla.
Aidha , Rais
Dk.Mwinyi ameiagiza timu kuu ya wataalamu ya Dira ya Maendeleo ya 2050 kukutana
na wadau mbalimbali kuhakikisha kazi ya kupokea maoni inakamilika kikamilifu
ili kuwa na Dira yenye kubeba maono ya wananchi wote.
Vilevile
Rais Dk. Mwinyi ameziagiza Tume za Mipango ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na ya Serikali ya Mapiduzi ya Zanzibar kuhakikisha wanaratibu zoezi la uhakiki
kwamba linafanyika kwa ufanisi wa hali ya juu pamoja na kuisambaza rasimu hiyo
kwa vyombo mbalimbali na kuweka mfumo halisi wa kupokea maoni.
Halikadhalika
Rais Dk. Mwinyi ameisisitiza timu hiyo ya Kitaalam kuhakikisha inamfikia kila
mwanchi kote nchini ili kutoa maoni bila kujali tofauti za dini, siasa, jinsia,
makundi maalum au eneo mtu analotoka kwani Rasimu hiyo ni ya Watanzania wote,
hivyo alieleza ni lazima ibebe maono yao ya miaka 25 ijayo.
Kwa upande mwingine,
Rais Dk. Mwinyi ameishauri timu hiyo ya kitaalamu kuandaa usimamizi mzuri wa
kukusanya maoni ya wadau kwa kuzunguka nchi nzima na kuandaa makongamano na
majadiliano na wadau.
0 Maoni