Serikali
imezitaka Taasisi na wadau wa sekta ya Utalii kushirikiana kwa pamoja katika
kukwamua rasilimali za wanyamapori kupitia shoroba mbalimbali nchini kwa
manufaa ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Wito huo
umetolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula (Mb)
wakati akifungua mkutano wa pili wa siku tatu wa jukwaa la wadau wa kuongoa
shoroba unaofanyika jijini Arusha.
Mhe.
Kitandula amesema jitihada zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau
wa uhifadhi zinaweza zisizae matunda ikiwa
jamii zinazoishi karibu na hizo
shoroba hazitashirikishwa kwenye uhifadhi kwani maarifa pamoja na uwakilishi
wao wa kuishi maeneo hayo ni kielelezo na kiungo muhimu cha uhifadhi endelevu.
Mhe.
Kitandula ameongeza kuwa wizara inaendelea kufanya juhudi kubwa ikiwemo
kutengeneza mkakati wa kufanya tathmini, kuweka viupaumbele pamoja na mpango
kazi wa miaka mitano (2022-2026) ambapo Shoroba 61 zimetambuliwa na 20
zimewekewa mkakati wa kipaumbele kwa
kuwa ziko hatarini kutoweka licha ya kuwa na umuhimu mkubwa wa kiikolojia na
uhifadhi endelevu.
“Ni hakika
Mjadala utatupa maarifa mapya, uzoefu mpya wenye kuleta suluhisho thabiti lenye
kuleta ustawi na utangamano kati ya
jamii zinazoishi karibu na shoroba pamoja na wanyama wanaotumia shoroba
hizo kama mapito,” amesema Mhe. Kitandula.
Kwa upande
wake Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo
Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba amesema kongamono hilo litasaidia
kuchukua hatua stahiki zitakazosaidia
kurejesha muunganisho wa wanyamapori na mifumo ya ikolojia ya wanyamapori kwa
ustawi wa jamii na Taifa kwa Ujumla.
“Kama wizara
tumetengeneza mpango mkakati wa kuongoa shoroba za wanyamapori ikiwemo
kuhakikisha muingiliano kati ya maeneo ya shughuli za binaadamu na njia za wanyama
linazibitiwa kikamilifu,” amesema CP Wakulyamba.
Katika hatua
nyingine CP. Wakulymba amewashukuru wadau wa kongamano hilo kwa kutenga muda
wao kujadili changamoto mbalimbali zinazokumba mapitio ya wanyama (shoroba) ili
kupata suluhisho muhimu kwa ajili ya ustawi wa uhifadhi endelevu.
Awali,
akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Wanyamapori wa Wizara ya Maliasili na
Utalii Dkt. Fortunata Msoffe amesema kuongolewa kwa shoroba za wanyamapori
itasaidia katika kuongezeka kwa vivutio vya utalii vitakayosaidia ukuaji wa
uchumi kupitia utalii na ongezeko la ajira kwa vijana ili kutimiza azma ya
serikali ya awamu ya sita chini ya rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutatua
changamoto ya ajira kwa vijana.
Kwa upande
wake Kaimu mwenyekiti wa kamati ya Kitaifa ya kuongoa shoroba za Wanyamapori
ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Ally Mfikirwa
amesema kukutana kwa wadau kupitia kongamano hilo kutaleta manufaa makubwa
ikiwemo kutafuta majibu ya kuondoa migongano kati ya binadamu na wanyamapori
lakini pia kuokoa maisha ya wanyamapori dhidi ya wananchi katika hifadhi zao.
0 Maoni