Wakala ya
Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Hanang imefanikiwa kurejesha
miundombinu ya barabara iliyoathiriwa na mafuriko ya tope, magogo na mawe mwishoni
mwa mwaka 2023.
Meneja wa
TARURA Wilaya ya Hanang, Mhandisi Paul Mlia amesema kwamba jumla ya Km. 74.7
ziliathirika zenye jumla ya madaraja 14, kati ya barabara hizo Km 19.7 ni za
Katesh mjini na Km 55 ni barabara za pembezoni mwa mlima Hanang.“Serikali
kupitia TARURA ilifanya tathimini ya uharibifu uliojitokeza katika miundombinu
hiyo ili kurejesha haraka huduma kwa wananchi,” alisema.
Aidha,
amesema maeneo mengine yaliyoathirika ni maeneo ya kijamii ikiwemo nyumba za
Ibada, soko la kateshi na makazi ya wananchi ambapo utekelezaji wake wa muda
mfupi walifanikisha uondoaji wa mawe, tope, magogo na kurejesha mawasiliano
katika barabara ya kateshi mjini yenye urefu wa Km 19.7 pamoja na uondoaji wa
matope ndani ya nyumba za wananchi 61.
"Kwa
upande wa wilaya ya Hanang tulipewa jukumu la utekelezaji wa mradi wa barabara
ya Dawar-Mogitu na barabara za mita eneo la makazi ya waathirika ya maporomoko ya tope Km. 13.50."
Pia, amesema
upande wa makazi mapya ya walioathirikia na mafuriko eneo la Walet, ambapo
walipewa jukumu la kujenga barabara kwa kiwango cha changarawe Km 13.5.
“Tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha waathirikia wa
mafuriko kwa kupata makazi mapya.”
Hata hivyo
ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu wameweza kuongezewa bajeti ya
ujenzi na matengenezo ya barabara kutoka milioni 800 hadi kufikia bilioni 2.3
hivi sasa na hivyo kuweza kujenga barabara ambazo zinaweza kupitika mwaka mzima
na hivi karibuni wanatarajia kuweka taa 27 katika mji wa Kateshi na kuwezesha
wananchi kufanya shughuli zao muda wote na hivyo kuwasaidia kukuza uchumi wao.
Nao wananchi
wa wilaya hiyo wameishukuru Serikali kupitia Wakala kwa kurejesha miundombinu
katika makazi yao kipindi cha mafuriko ya tope.
Mkazi wa
Hanang, Bw. Rogat Petro amesema wanaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwani
wilaya yao imenufaika na mambo mengi licha ya wilaya hiyo ni ya muda mrefu na
hivyo kupatiwa barabara katika kata za pembeni ni jambo jema.
“Tunamshukuru
Mhe. Rais ametusaidia hasa kipindi cha mafuriko kwa kutuma viongozi wake na kuweza kuturejeshea mawasiliano na hadi
sasa watu wote tunaendelea na shughuli zetu za kila siku.”
Amemalizia
kusema kwamba wananchi wa Hanang wanaheshimu miundombinu ya Serikali na
kwamba wana umoja na wapo tayari kulinda
uwekezaji wote uliowekezwa na Serikali.
0 Maoni