Naibu Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Zainab Katimba (Mb) amemtaka Mkandarasi na
Mtaalamu Mshauri anayetekeleza Mkataba wa Ujenzi wa miundombinu inayoratibiwa
na mradi wa TACTIC wilayani Kahama Mkoani Shinyanga kukamilisha haraka ujenzi
huo kulingana na matakwa ya mkataba ili wananchi wanufaike kikamilifu na
uwekezaji huo unaosimamiwa na Serikali kupitia TAMISEMI.
Naibu Waziri
Katimba amesema hayo jana Desemba 04, 2024 mjini Kahama, Shinyanga, wakati wa
utiaji saini mkataba wa ujenzi wa kituo kikuu cha mabasi eneo la Mbulu, ujenzi
wa soko la Sango pamoja na ujenzi wa kituo kidogo cha mabasi na Soko la
Wajasiriamali wadogo eneo la Zongomera wilayani Kahama, akisema kukamilika kwa
miradi hiyo kunaenda kukuza na kuimarisha uchumi wa mwananchi na kukuza pato la
mkoa wa Shinyanga.
Mhe. Katimba
ametoa kauli hiyo mara baada ya kupata malalamiko kadhaa kutoka kwa viongozi
mbalimbali mkoani Shinyanga, wakilalamikia mwenendo usioridhisha wa Mkandarasi
M/S Sichuan Road and Bridge (Group) Corporation Ltd anayetekeleza ujenzi wa
barabara za mjini, barabara ya kuingia kituo cha wajasiriamali cha Zongomela
pamoja na mitaro ya kutiririsha maji ya mvua kwenye Halmashauri ya mji wa
Kahama.
Kufuatia
maelekezo hayo, Mhe. Katimba ametembelea na kukagua miradi hiyo inayolalamikiwa
na kupata maoni ya wadau mbalimbali, akiahidi Kumshauri Waziri wa Nchi-
TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa (Mb) kuhusu hatua za kuchukua kwa Mkandarasi
huyo anayesuasa katika utekelezaji wa mradi huo kwa kwenda kinyume na mkataba
na hivyo kusababisha kuchelewa kwa tija ya uwekezaji huo.
Katika hatua
nyingine, Naibu Waziri Katimba amemuagiza Mtaalamu mshauri na Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Kahama kuhakikisha kuwa mikataba inasimamiwa vizuri
ili kuwezesha kukamilika ndani ya muda uliopangwa, kwa ubora tarajiwa huku
thamani ya fedha iliyotumika ikitakiwa kuonekana kwa ukamilifu wake.
Aidha, Mhe.
Katimba alisema uboreshaji wa miundombinu ya barabara unaofanywa na Serikali ya
Rais Samia Suluhu Hassan kupitia TARURA, umepelekea ongezeko kubwa la bajeti ya
TARURA kutoka Bilioni 275 hadi Bilioni 710 kwa mwaka ikiwa ni utekelezaji wa
Ilani ya CCM ya mwaka 2020 inayoelekeza kuhusu maboresho ya miundombinu ya
usafiri na usafirishaji ili kuchochea shughuli za kiuchumi.
Mhe. Katimba
pia amesema uboreshaji huo umewezeshwa na wadau mbalimbali ikiwemo Benki ya
Dunia yenye kutekeleza miradi kadhaa ikiwemo ya TACTIC suala linalosaidia
kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, kuibua fursa mpya za ajira pamoja na
kustawisha pato la wananchi na la Manispaa, Miji na Majiji ya Tanzania.
Kufuatia
jitihada hizo, Mhe. Katimba amewataka wananchi wa Mkoa wa Shinyanga na maeneo
mengine inapotekelezwa miradi ya TACTIC kulinda miundombinu hiyo ili
kuhakikisha kuwa inatumika na jamii kwa muda mrefu.
"Wananchi
tuna wajibu wa kuilinda miradi hii inayojengwa kwa gharama kubwa ili kuleta tija kwa wananchi kulingana na
matarajio na malengo ya mikataba ya utekelezaji wa miradi,"
alisema Mhe. Katimba.
0 Maoni