Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameeleza amefurahishwa kwake na uendeshaji wa UDSM Marathon na kusema kuwa inasaidia kufanikisha malengo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuendelea kutoa elimu bora na kuboresha mazingira ya wanafunzi.
Dkt. Biteko
amesema hayo leo Desemba 7, 2024 mara baada ya kushiriki mbio hizo za Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM MARATHON) zilizofanyika chuoni hapo.
“ Ni dhahiri
kwamba mbio hizi zimekuwa muhimu kwa Chuo hiki na jamii kwa ujumla. Tukio hili
limeleta pamoja wadau mbalimbali na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika juhudi
za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza
“Natambua kwa misimu mitano mbio hizi zimekua zikichangia katika ujenzi wa
Kituo cha Wanafunzi kinachojengwa hapa katika Kampasi Kuu ya Mwalimu Nyerere
Mlimani. Ujenzi wa kituo hiki ulianza kwa michango kutoka kwa wahitimu wa Chuo
Kikuu cha Dar Es Salaam na washirika mbalimbali wa maendeleo ya elimu ambapo
jumla ya shilingi bilioni 4.4 zimechangwa kutoka kwa wadau.”
Aidha, awamu
ya kwanza ya ujenzi imekamilishwa kwa kutumia fedha za ndani na hivyo kazi kubwa iliyobaki ni kukamilisha
awamu ya pili ili kutimiza ndoto ya kuwa
na Kituo cha Wanafunzi kitakachowezesha wanachuo kuwa na maeneo ya
kujifunzia na kupata nafasi ya kukuza
vipaji vyao.
Ujenzi wa
awamu ya pili unahitaji shilingi bilioni 3.3 na hivyo kufanya gharama za ujenzi
kwa awamu hiyo kufikia shilingi bilioni 9.4 badala ya shilingi bilioni 6
zilizokadiriwa awali ambazo zimebadilika kwa sababu mbalimbali.
Akiwahakikishia
ushiriki wake katika kufanikisha ukamilishaji wa ujenzi wa Kituo Dkt. Biteko
amesema, “Nataka niwatoe wasiwasi kuwa jambo hili ni letu sote kwa kuwa majengo
haya yatatumika kwetu sote. Nalibeba suala hili kwa uzito wake ili
kilichoahidiwa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi kipatikane kwa wakati.”
Pia, ametoa
wito kwa wadau mbalimbali kuunga mkono jitihada za kuwezesha mbio hizo
kufanyika kwa ustadi mkubwa na kwa kuwa zimeonesha kupitia mshikamano, wanaweza
kufanikisha malengo makubwa ya kijamii na kielimu. Sambamba na kuhimiza uongozi wa Chuo kuandaa namna ya kukutanisha
wadau zaidi ili kuchangia fedha za kukamilisha ujenzi wa kituo.
Vilevile,
Dkt. Biteko amempongeza Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Rais wa Awamu
ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa usimamizi wake katika shughuli za
maendeleo ya Chuo hicho.
Kwa upenda
wake, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Rais Mstaafu Mhe. Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete amesema kuwa Chuo hicho kinathamini mchango wa Serikali katika
ujenzi wa Kituo hicho cha wanafunzi.
Naibu Makamu
Mkuu wa Chuo cha Dar es Salaam (Utawala na Fedha), Prof. Bernadeta Kilian
amesema Chuo hicho kilianzisha ujenzi wa kituo cha wanafunzi kwa ajili ya
kupumzika na kukuza uwezo wa kubuni au kupata mawazo Mapya.
Na. Ofisi ya
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni