Tutaingia tena kuwania nafasi ya WHO- Rais Samia

 

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Tanzania itaingia tena kwenye ushindani wa kuwania nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika, baada ya kumpoteza Mkurugenzi Mteule wa shirika hilo marehemu Dkt. Faustine Engelbert Ndugulile.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Desemba 2, 2024 Jijin Dar es Salaam, katika hotuba yake fupi aliyoitoa wakati wa kuaga mwili wa Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Marehemu Dkt. Faustine Engelbert Ndugulile, katika viwanja vya Karimjee.

“Lakini niseme Dkt. Faustine katika safari yake hii ya mwisho ameweka heshima kubwa kwa nchi yetu kwa kupata nafasi ile, naniseme kwamba Mungu amechukua amana yake lakini kwetu sisi ni kwenda, tutawania tena nafasi ile,” alisema Rais Samia na kuongeza, “Tutatafuta Mtanzania mwenye sifa zinazoweza kushindana na ulimwengu tutaingia tena na tutaweka nguvu ileile ili kuweka heshima ya nchi yetu.”

Awali Mchungaji Josephat Gwajima amemzungumzia aliyekuwa mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile, akisisitiza umuhimu wa kuelewa tafsiri sahihi ya maisha na wajibu wa kila mtu duniani.

Akizungumza kwa niaba ya wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mchungaji Gwajima amesema, “Ipo sababu ya kupata tafsiri sahihi ya umuhimu wa maisha na maisha ni nini. Janga si kifo; mtu mmoja alipata kusema janga ni kuwa hai wakati wengine wanakufa na wewe hujui kwa nini uko hai.”

Dkt. Gwajima amesema kuwa kila mtu amepewa misheni tofauti na Mungu, ikiwemo ya kisiasa, kiuchumi, au kiroho, ambayo inapaswa kutimizwa kwa wakati.



Chapisha Maoni

0 Maoni