Katika kuendelea kupanua wigo wa upatikanaji wa elimu ya Sekondari, Jimbo la Musoma Vijijini lililopo Wilaya ya Musoma Vijijini Mkoani Mara linatarajia kufungua shule za Sekondari mpya sita ifikapo mwakani 2025.
Jimbo hilo ambalo mbunge wake ni Prof. Sospeter Muhongo,
limejiwekea vipaumbele kadhaa ambapo elimu ni kipaumbele namba moja ambacho
kimekuwa kikitekelezwa kwa kasi yenye kuridhisha.
Taarifa iliyotolewa na ofisi ya mbunge wa jimbo la Musoma
Vijijini imetaja Sekondari hizo sita mpya kuwa ni Rukuba Island, Nyasaungu,
Muhoji, Butata, Sekondari ya Ufundi ya Nyamrandirira na David Massamba Memorial.
Sekondari hizo zimejengwa kwa michango ya fedha na
nguvukazi kutoka kwa wanavijiji na viongozi wao, huku Serikali nayo ikitoa
shilingi milioni 584, kwa kila sekondari kwa ajili ya ujenzi wake.
Taarifa hiyo imesema kwamba pamoja na kukamilika kwa Sekondari
hizo sita mpya, tayari wamepata vibali vya kuanza kujenga Sekondari mpya sita
katika vijiji Chitare, Kataryo, Kiriba, Mmahare, Musanja na Nyambono.
Mbunge wa Musoma Vijijini Prof. Sospeter Muhongo akiwa kwenye jengo la darasa la moja ya za Sekondari zinazojengwa katika jimbo hilo, ambazo zinatarajiwa kuanza kutumika kuanzia mwakani 2025.
0 Maoni