Askofu wa KKKT, Dayosisi ya Karagwe Dkt. Benson Bagonza
Habari za maskini kutajirisha matajiri si ngeni kwetu.
Tumewaona wakulima maskini wakitajirisha matajiri, waumini maskini
wakiwatajirisha wahubiri, Boda boda maskini wakiwatajirisha wauza pikipiki na
maaskari barabarani na wapiga kura maskini wakitengeneza viongozi matajiri
lakini maskini hawa hatuwezi kuwaita kuwa ni Yesu Kristo.
Wakati huo huo hatuwaoni matajiri wanaowatajirisha
maskini tunachokiona ni atajiri wanaodhani wana bidii na akili na maskini
wanaoambiwa ni wavivu na hawana akili. Kwao hawa matajiri kutajirika ni akili
na ujanja.
Hawa matajiri huwaona maskini kuwa ni wavivu na wasio na
akili. Ukweli ni kwamba utajiri na umaskini vina uhusiano wa karibu sana na
mara nyingi uhusiano huu umejengwa katika unyonyaji.
Kuzaliwa kwa Yesu kulileta picha tofauti.
Yeye alikuwa tajiri ili maskini wawe matajiri na
alizaliwa katika hali ya umaskini ili sisi tuwe matajiri. Maskini na matajiri
wote wana nafasi katika kuzaliwa kwa Yesu lakini kwa namna pekee Yesu alizaliwa
kwa ajili ya waliokosa tumaini na kukosa mtetezi.
Jamii yetu inalo la kujifunza kutoka kwa Yesu Kristo.
Tunaalikwa kumtazama Yesu katika sura ya wanaoteseka.
Mtazame Yesu katika sura ya Mpalestina anayeteketezwa na
mabomu ya nchi tajiri.
Mtazame Yesu kama mtu wa Ukraine anayekaangwa kwa mabomu
ya ubabe wa Urusi . Mtazame Yesu kama mwanaharakati anayepigania haki ya
Kidemokrasia anayetekwa na kupotezwa kama gaidi.
Mtazame Yesu kama mtu maskini anayelazimika kununua haki
zake katika ofisi za umma. Mtazame Yesu kama mwananchi maskini anayelazimika
kununua uponyaji na wokovu wake. Mtazame Yesu kama mtu asiye mwanachama wa
chama chochote anayepoteza haki ya kuchaguliwa kuwa kiongozi na kuishia kuwachagua
wengine wamwongoze.
Na haya yanapotokea mtazame Yesu katika sura ya jamii
inayokosa haki wakati watu wote wako kimya.
0 Maoni