WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa leo Desemba 30, 2024 amemwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye mazishi ya Mheshimiwa Mwanaisha Kwariko ambaye alikuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Akitoa Salama pole kwa waombolezaji nyumbani kwa marehemu
Kondoa, Mkoani Dodoma, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Rais Dkt. Samia
ameguswa na kifo cha Mheshimiwa Mwanaisha kwani alikuwa ni moja ya majaji wa
mahakama ya rufani wenye uwezo mkubwa katika nafasi zote alizozitumikia.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Marehemu Mheshimiwa
Mwanaisha alikuwa kiongozi aliyetekeleza wajibu wake kwa weledi na uadilifu
“Msiba huu kwetu ni mzito, jukumu letu Wanakondoa, Watanzania, Majaji na
wajumbe wa Tume ni kuendelea kumuombea kwa Mwenyezi Mungu.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa kila mmoja
kuenzi yote mazuri aliyoyafanya Mheshimiwa Mwanaisha katika kipindi chake chote
cha utumishi wa umma kwani kufanya hivyo kutakuwa ni njia nzuri ya kuweka
kumbukumbu ya kazi zake.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahimu
Juma amesema kuwa Mheshimiwa Mwanaisha Kwariko aliishi kiapo cha Uhakimu kwa
kutoa huduma kwa wananchi ikiwemo kutatua migogoro kwa uadilifu bila upendeo
wowote.
“Mheshimiwa Mwanaisha alikuwa na ubinadamu na utu, maisha
yake yalikuwa ni yakusaidia watu wengine, sisi tunamshukuru Mwenyezi Mungu
kwani uhai wake umetusaidia sana katika shughuli mbalimbali za kimahakama.”
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya
Uchaguzi Mhe. Jaji (Rufani) Jacobs Mwambegele amesema kuwa Mheshimiwa Mwanaisha
ameondoka katika kipindi ambacho tume ilikuwa inamuhitaji hasa katika kipindi
hiki ambacho tume hiyo ipo katika mchakato wa
kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura kuelekea uchaguzi mkuu wa
Rais, Wabunge na Madiwani
“Tumempoteza Mheshimwa Mwanaisha tukiwa kwenye mzunguko
wa nane wa zoezi la kuboresha daftari na tukiwa tunaingia kwenye mzunguko wa
tisa utakaohusiaha mikoa minne Rukwa, Songwe, Njombe na Ruvuma, pia mara zote
alitoa ushauri wenye weledi wa hali ya juu katika kuhakikisha tume inatekekeza
majukumu yake kwa kuzingatia katiba sheria kanuni na taratibu.”
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amesema
kuwa Mheshimiwa Mwanaisha alikuwa ni kiongozi mwenye msimamo na mtetezi wa
masuala ya wanawake, “alibobea katika eneo ambalo alikuwa anafanyia kazi, sisi
wanadodoma tutamkumbuka kwa machango wake mkubwa kwenye masuala ya maendeleo.”
Marehemu Mheshimiwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Mwanaisha
Kwariko alifariki Desemba 27, 2024 nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimpa pole Mwajuma Mafita
ambaye ni Mama wa marehemu Mheshimiwa Mwanaisha Kwariko, aliyekuwa Jaji wa
Mahakama ya Rufani. Waziri Mkuu alimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
katika mazishi hayo, Kondoa Mkoani Dodoma. Desemba 30, 2024 (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiweka udongo kwenye kaburi
la Mheshimiwa Mwanaisha Kwariko ambaye alikuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.
Mheshimiwa Majaliwa alimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mazishi
yaliyofanyika Kondoa, mkoani Dodoma, Desemba 30, 2024 (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu)
0 Maoni