Utegemezi wa visima vya maji visivyokuwa vya kitaalamu na
kutembea umbali mrefu kufuata maji katika Wilaya ya Bukombe mkoani Geita
umepungua katika kipindi cha Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan.
Mafanikio haya yamechagizwa na miradi mbalimbali ya maji
iliyotekelezwa kwa ufanisi kufuatia azma ya Mbunge wa Jimbo la Bukombe ambaye
pia ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko
kutatua changamoto ya maji katika jimbo hilo.
Dkt. Biteko amesema kwamba mafanikio hayo yametokana na kufanya
kazi kwa pamoja Mbunge, Madiwani, Wenyeviti wa Vitongoji pamoja na viongozi wa
Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kusukuma mbele wilaya iendelee pamoja na
maendeleo ya kijimbo yafanikiwe.
Nao wakazi wa Bukombe wameishukuru Serikali ya awamu ya
sita pamoja na mbunge wao kwa kuwatatulia kero ya maji, ambapo wamesema awali
iliwalazimu kupata maji katika umbali mrefu ila sasa hivi wanapata huduma ya
maji kwa karibu sana.
“Tunamshukuru sana mbunge wetu Dkt. Doto Biteko kwa kutuona
hapa Katome tulikuwa tunahangaika maji, wakinamama tulikuwa tunafuata maji kwa
umbali mkubwa sana, hata watoto wetu wakike waliipitia changamoto hii," amesema
Coletha Msemelwa Mkazi wa Kijiji cha Kanembwa.
Wanaume nao hawakuachwa na changamoto hiyo kama
anavyosema hapa Aloyce Makala Mkazi wa Kata ya Busonzo, “Lakini pia kunahuduma
za msingi kwa wanaume tulikua tunazikosa mida ya asubuhi, unamka mwenzio pembeni
hayupo katoka kwenda kutafuta maji.. lakini sasa hivi angalau, ninavyozungumza
hivi nadhani wanaume wezangu mnanielewa.”
0 Maoni