Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limesema kuwa watu watano
wa familia moja wamekufa kwa kupigwa na radi wakiwa kwenye kambi ya kuchungia ng'ombe
wakati wakiwa wamelala Wilaya ya Chunya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Benjamin Kuzaga
amesema tukio hilo lilitokea tarehe 29/12/2024 saa 8:30 usiku katika Kitongoji
cha Nkangi kilichopo Kijiji cha Isangawana, Kata ya Matwiga, Tarafa ya
Kipembawe, Wilaya ya Chunya.
“Watu hao watano wa familia moja ya Masiganya Scania (39)
anayejishughulisha na ufugaji, mkazi wa Nkangi walifariki dunia baada ya
kupigwa radi kwenye kambi ya kuchungia ng'ombe wakati wakiwa wamelala,” amesema
Kamanda Kuzaga.
Amewataja waliofariki kwenye tukio hilo kuwa ni Balaa
Scania (28), Kulwa Luweja (17), Masele Masaganya (16), Hema Tati (10) pamoja na
Manangu Ngwisu (18) wote wakazi wa Kijiji cha Nkangi.
Aidha, katika tukio hilo watu wengine watano walijeruhiwa
ambao ni Gulu Scania (30), Manyenge Masaganya (13), Seni Solo (13), Paskali
Kalezi (16) na Huzuni Kalezi (19) wote wakazi wa Kijiji cha Nkangi.
Kamanda Kuzaga amesema chanzo cha tukio hilo ni mvua
kubwa iliyonyesha usiku ikiambatana na radi hivyo kusababisha vifo vya watu
watano na wengine watano kujeruhiwa.
Majeruhi walikimbizwa katika Kituo cha Afya Isangawana
kwa matibabu na walitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani baada ya hali zao kuwa
nzuri.
0 Maoni