Jeshi la
Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni limetembelea na kukabidhi zawadi kwa uongozi
wa Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila kwa lengo la kuwasaidia wagonjwa
wasio na uwezo waliolazwa hospitalini hapo.
Akikabidhi
msaada huo kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Mkuu wa
Polisi Jamii mkoa huo, ACP-Ally Wendo amesema jeshi hilo limeona litoe msaada
kwa wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo kwa kutambua kuwa wapo wagonjwa
ambao hawana uwezo kabisa.
“Zawadi hizi
zimetoka kwa Polisi Mkoa wa Kinondoni, tumeona tutoe kile kidogo tulichonacho
kwa ajili ya kuwasaidia ndugu zetu wanaopata matibabu hapa, nimeambatana na OCD
Kimara pamoja na OCS Kimara (Gogoni), tunaamini zawadi hizi zitaongeza
matumaini kwao,” ameongeza ACP Wendo.
Kwa upande
wake Kamanda wa Polisi wilaya ya Kinondoni (OCD) SSP-Deogratias Massawe amesema
pamoja na kukabidhi msaada huo wamepata fursa ya kupata elimu ya namna ya
kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza ambayo yamekuwa tishio kwa siku za
karibuni.
Naye, Mkuu
wa Idara ya Ustawi wa Jamii Bw. Emmanuel Mwasota amelishukuru Jeshi la Polisi
Mkoa wa Kinondoni kwa msaada huo na kuongeza kuwa hospitali hiyo inapokea
wagonjwa kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, ambapo wengine ni wale wanaopata
ajali barabarani ambao wengi wao ndugu zao hawajulikani na hufikishwa
hospitalini wakiwa hawana kumbukumbu sawasawa.
Pamoja na
maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Tanzania Bara, Jeshi hilo limetoa msaada huo
ikiwa ni kilele cha Siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia.
0 Maoni