Nondo atakapopona ataongea yote- Zitto Kabwe

 

Kiongozi Mkuu Mstaafu wa ACT Wazalendo Zitto Kabwe amemtembelea Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa chama hicho Abdul Omary Nondo katika hospitali ya Aga Khan na kusema kuwa hali yake bado si nzuri na anaendelea na matibabu.

Zitto amesema kwamba kwa sasa Nondo anaendelea na matibabu na hali yake itakapotengemaa ndipo ataweza kuelezea tukio hilo lililomkuta, “Tunaamini hapa alipo yupo katika hospitali sahihi kwa matibabu yake atakapopona ataongea.”

Nondo alitekwa jana leo alfajiri katika stendi ya Magufuli eneo la Mbezi Louis wakati akiwasili kutokea mkoani Kigoma kwa usafiri wa basi la Saratoga lenye namba za usajili T 221 DKB.

Kufuati tukio hilo Jeshi la Polisi limesema kwamba linafuatilia tukio la kutekwa Nondo baada ya kufungua jalada, hata hivyo jana usiku Nondo alipatikana akiwa ametelekezwa kwenye fukwe ya Coco huku akiwa na maumivu makali.

Taarifa ya Polisi iliyotolewa leo Desemba 2, 2024 na msemaji wake, David Misime imesema  baada ya kutelekezwa katika fukwe hizo, aliomba msaada wa bodaboda kumfikisha katika ofisi za chama chake Magomeni, Dar es Salaam.

"Desemba mosi, 2024 majira kama saa nne na nusu usiku Abdul Omary Nondo ambaye tulikuwa tunamtafuta kwa kushirikiana na watu mbalimbali, wakiwepo viongozi wake wa chama cha ACT Wazalendo baada ya kukamatwa na kuchukuliwa kwa nguvu pale kituo cha mabasi cha Magufuli, ameeleza alitelekezwa maeneo ya fukwe za Coco (Coco Beach) Kinondoni, Jijini Dar es Salaam na watu asiowafahamu.

"Baada ya kutelekezwa alisimamisha bodaboda na kumwelekeza amfikishe katika ofisi za chama chake zilizopo Magomeni, Jijini Dar es Salaam na walifika muda wa saa tano usiku,” imeeleza tarifa hiyo na kuongeza kuwa alionana na viongozi wake na kupelekwa hospitali kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake.

Chapisha Maoni

0 Maoni