WAZIRI wa
Madini Mhe. Anthony Mavunde anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye mnada wa madini
ya vito
unaotarajiwa kufanyika katika mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro
mkoani Manyara, ili kuyaongezea thamani madini hayo.
Mnada huo
ambao ulisimama kwa muda, umepangwa kufanyika tena kwa mara ya kwanza Desemba
14, 2024.
Akizungumza
leo Desemba 12, 2024, Mheshimiwa Mavunde amesema madini ya vito, yanafanyiwa
mnada kama mkakati wa kuyatangaza na kuyaongezea thamani kimataifa.
Mhe. Mavunde amesema utaratibu wa kufanya mnada
huo ni jitihada za Serikali za kudhibiti utoroshwaji wa madini hayo nje ya nchi
na pia kuwasaidia wachimbaji kuuza madini yao kwa bei ya ushindani inayoendana
na soko la dunia.
Amesema,
mnada huo utashirikisha wanunuzi kutoka ndani na nje ya nchi na atakayenunua
madini hayo katika mnada ni atakayeshinda bei iliyowekwa.
“Mnada huu
utaendeshwa kwa usalama mkubwa kwa kuwa madini hayo hususan Tanzanite yana
thamani kubwa. Serikali imeimarisha ulinzi ili kujihadhari na watu wasio
waaminifu,”amesema Waziri Mavunde.
Aidha,
amesema mnada huo utaiwezesha Serikali kupata mrabaha stahiki na kodi kwa uwazi
ili kuchangia pato la Taifa na kuimarisha ulinzi na usalama kwa wauzaji,
wanunuzi na mali zao.
Minada kama
hiyo pia hufanyika kwa nchi za Afrika zenye madini ya vito kama vile Zambia
(emerald), Zimbabwe (almasi) na Afrika Kusini (almasi).
0 Maoni