Zaidi ya TZS
Milioni 220 zilizotolewa na Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Mamlaka ya
Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Kwa ajili ya maboresho ya miundombinu
ya utalii ndani ya bustani ya wanyamapori hai "Tabora ZOO" zimekuwa
chachu ya kuchechemua utalii wa ndani Mkoani Tabora.
Hayo
yamesemwa jana Desemba 12, 2024 na Afisa Wanyamapori Mkuu kutoka Kanda ya
Magharibi ya TAWA Jovin Nachihangu wakati akiongea na waandishi wa habari
kutoka vyombo mbalimbali vya habari ndani ya bustani hiyo ya wanyamapori hai.
"Kabla
ya maboresho ya miundombinu ya utalii TAWA tulikuwa tunakusanya TZS Millioni 1
Kwa Mwaka, lakini baada ya maboresho katika kipindi hiki cha miaka 3 TAWA
inakusanya kupitia bustani hii kiasi kisichopungua TZS Millioni 50 Kwa Mwaka na
bado tunaendelea kuhakikisha kwamba mapato yanaendelea kuongezeka,"
amesema Jovin.
Aidha, Jovin
amebainisha miundombinu iliyoboreshwa ndani ya bustani hiyo kuwa ni jengo la
wananchi kupata taarifa za vivutio vya utalii vinavyopatikana katika bustani
hiyo na Kanda ya Magharibi Kwa ujumla (Visitors Information Centre - VIC), vyoo
vya kisasa Kwa ajili ya wageni na mabanda ya wanyamapori walao nyama (Simba,
Chui, Duma n.k).
Kwa upande
wake Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja amemshukuru Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan Kwa kuiwezesha Taasisi ya TAWA
kupata fedha za kuboresha miundombinu ya utalii katika bustani hiyo, jambo
ambalo amesisitiza kuwa limekuwa chachu ya kuchechemua utalii wa ndani katika
Mkoa wa Tabora.
Maganja
amesema katika kipindi cha miaka mitatu kabla ya maboresho walikuwa wakipata
wageni wachache katika bustani hiyo.
Amesema
katika kipindi cha Mwaka 2021/22 bustani hiyo ilipokea wageni 308, na Kadri
maboresho yalivyozidi kufanyika Taasisi hiyo ilishuhudia ongezeko la wageni
ambapo Mwaka 2022/23 walipokea wageni zaidi ya 6,300 na katika kipindi cha
Mwaka 2023/24 wameweza kupokea zaidi ya wageni 10,700 Jambo ambalo linaleta
matumaini makubwa.
Naye Diwani
wa Kata ya Kitete Mhe. Mussa Kayolo amesema Tabora ZOO imekuwa ni kivutio
kikubwa Kwa wakazi wa Mkoa wa Tabora kutokana na upekee wake wa kuwa katikati
ya Manispaa ya Tabora, uwezo wa kufikika Kwa urahisi na wingi wa rasilimali
wanyamapori na vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo bustanini humo.
Mhe. Kayolo
ametumia fursa hiyo kuwakaribisha na kuwahamasisha wawekezaji wote wenye kiu ya
kuwekeza, wawekeze katika bustani hiyo.
0 Maoni