Naibu Katibu
Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia Utalii Nkoba Mabula amesema
zaidi ya asilimia 90 ya Wapanda Mlima zaidi ya 250 waliojitokeza kupanda Mlima
Kilimanjaro ili kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara wamefika katika
kilele hicho usiku wa kuamkia Desemba 09, 2024.
Ndg. Nkoba
ameyasema hayo jana Desemba 10, 2024 katika lango la Marangu lililopo mkoani
Kilimanjaro wakati wa hafla ya kuwapokea wapandaji hao walioianza safari ya
kukwea jabali hilo tarehe 03 hadi 05/12/2024 wakipitia njia tofauti za Lemosho,
Machame na Marangu.
Rekodi hiyo
imevunjwa kutokana na wingi wa wapandaji hao kufika katika kilele cha Paa hilo
la Afrika lenye urefu wa mita 5,895 kutoka usawa bahari. Mlima Kilimanjaro ni
miongoni mwa milima iliyotokana na mlipuko wa Volcano, ukivuta watalii wengi
kutokana na upekee wake wa kuwa na barafu kileleni tofauti na milima mingine
iliyoko ukanda wa kitropiki.
Akiwa katika
hafla hiyo, Naibu Nkoba alisema, “Licha ya wapandaji wengi kufika kileleni, pia
kampeni hiyo imehusisha wapanda mlima kutoka mataifa mengine ya Marekani,
Austria na China huku ikijumuisha kundi la watu wenye uhitaji maalumu tofauti
na miaka ya nyuma.”
Hata hivyo,
kampeni hiyo ilijumuisha kundi la wazawa waliopanda kwa kukimbia kwa kutumia
masaa 13:02, wengine kutembea kwa kasi na kutumia siku moja tofauti na wapanda
mlima wengi waliotumia siku 8 Lemosho, siku 7 Machame na siku 6 Marangu.
Naye, Balozi
Dkt. Mahadhi Maalim anayeiwakilisha Tanzania nchini Malayasia na kiongozi wa
jopo la mabalozi waliopanda alisema ujio wao utaongeza weledi wa kuujua zaidi
mlima huo na kunadi vivutio zaidi ya kivutio cha kupanda mlima huo ikiwemo
utalii wa Parachuti, kupanda kwa baiskeli na zao la kupanda kwa kukimbia kama
walivyoshuhudia kipindi hiki.
Aidha ,
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania(TANAPA)
Jenerali (Mstaafu) George Waitara aliwapongeza “Guide”, Wapishi na Wapagazi
alimaarufu Wagumu kwa jitihada na uzalendo waliouonyesha kufanikisha zoezi zima
la kupanda mlima huo.
“Juhudi zenu
na Uzalendo umekuwa nguzo ya kufanikisha zoezi la kupanda mlima huu. Hata hivyo
nyinyi ndio chachu ya kukuza utalii huu wa kupanda Mlima Kilimanjaro na sekta
nzima ya utalii hususani kwa kanda hii ya Kaskazini,” alisema Jenerali (Mst.) Waitara.
Kwa upande
wake, Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara TANAPA Massana
Mwishawa aliwasihi watanzania kuendelea kutunza Mlima Kilimanjaro kwa kutokata
miti ili kupunguza kasi ya kuyeyuka barafu unaosababishwa na mabadiliko ya
tabianchi na uharibifu wa mazingira unaofanywa na binadamu.
"Mlima
Kilimanjaro ni tunu ya Taifa na ni chanzo ajira kwa wananchi wanaoishi katika
ya Kaskazini, hivyo kuharibika kwa mazingira yake, hakutoathiri Tanzania tu
bali pia nchi za Kenya, Uganda, Rwanda na Afrika Kusini ambao hutegemea kuleta
wageni na kujipatia kipato”, aliongeza Kamishna Mwishawa.
Hafla hiyo
adhimu ya kuwapokea wapanda mlima Kilimanjaro kwa ajili ya kumbukumbu ya
Maadhimisho ya miaka 63 ya uhuru wa Tanganyika kupitia kampeni ya “TWENZETU
KILELENI” imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, ikiweno Naibu katibu
Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii,
Mabalozi kutoka nchi mbalimbali,Jeshi la Wananchi (JWTZ), Bodi ya Wadhamini
TANAPA, Viongozi waandamizi wa vyama vya Siasa, taasisi mbalimbali na viongozi wa dini.
Na. Happiness Sam/Kilimanjaro
0 Maoni