Katibu Mkuu
wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi ameelekeza kuendelea kwa
matumizi ya teknolojia mbalimbali katika ulinzi wa rasilimali ya wanyamapori.
Dkt. Abbasi
ameyasema hayo leo Desemba 10, 2024, katika kikao na watumishi wa Mamlaka ya
Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) kilichofanyika katika Makao Makuu ya TAWA
Mkoani Morogoro.
"Tuendelee
kutumia teknolojia za kisasa katika ulinzi wa rasilimali ya wanyamapori,"
amesema Dkt. Abbasi.
Aidha, Dkt.
Abbasi ameipongeza TAWA kwa utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa katika
ziara yake ya kikazi Mkoani Ruvuma mnamo mwezi Septemba ya kununua ndege nyuki
kwa ajili kudhibiti wanyama wakali na waharibifu.
"Nimefurahi
kuona mmeanza kutekeleza maelekezo ya Rais ya kununua ndege nyuki na hapa TAWA
nimeona kazi imeanza," ameongeza Dkt. Abbasi.
Vilevile,
Dkt. Abbasi alitoa pongezi kwa TAWA kwa ujenzi wa vizimba sambamba na ujenzi wa
mabwawa katika Hifadhi ya Rungwa na Makuyuni ambao utasaidia kupunguza
changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wanyamapori.
Kwa upande
wake, akimwakilisha Kamishna wa Uhifadhi TAWA, Kaimu Naibu Kamishna wa
Uhifadhi, Mlage Kabange alimshukuru Katibu Mkuu kwa ujio wake na amesema kuwa
maelekezo yaliyotolewa yatatekelezwa kwa asilimia mia moja.
" Sisi
kama TAWA ni jadi yetu kutekeleza maelekezo bila kupindisha" amesema
Kamishna Kabange.
Kuhusu
matumizi ya teknolojia, Kamishna Kabange ameongeza kuwa TAWA imenunua ndege
nyuki 11 kwa ajili ya shughuli za uhifadhi na itaongeza nyingine zaidi,
sambamba na kutafuta teknolojia zingine zitakazosaidia katika shughuli za
uhifadhi.
Awali,
Dkt.Abbasi alipata wasaa wa kuangalia onesho la matumizi ya ndege nyuki katika
kumrudisha tembo hifadhini sambamba na kukabidhiwa kombe la SHIMMUTA kwa upande
wa mashindano ya Kamba na Riadha.
Na. Joyce Ndunguru- Morogoro



0 Maoni