Mkazi wa Nkalalo wilayani Kwimba mkoani Mwanza, Nicholaus
James (21) amehukumiwa kifungo cha miaka 30 gerazani baada ya kukutwa na hatia
ya kumbaka mwanafunzi wa kidato cha nne (jina linahifadhiwa) wa Sekondari ya
Taro wilayani humo.
Katika kesi hiyo ya Jinai namba 22882/2024, James ametiwa
hatiani na Mahakama ya wilaya Kwimba kwa kosa la kumbaka binti ambaye
utambulisho wake unahifadhiwa kwa sababu za kisheria (19) mwanafunzi wa kidato
cha 4 shule ya sekondari Taro.
Hukumu hiyo ilisomwa jana tarehe 16/12/2024 na Hakimu
Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Kwimba, John Jagadi mbele ya
mwendesha mashtaka wa Serikali Juma Kiparo.
Awali, Mwendesha Mashtaka Juma Kiparo aliieleza Mahakama
kwamba mshtakiwa alitenda kosa hilo tarehe 07.08.2024, katika Kijiji cha
Nkalalo, wilaya ya Kwimba kinyume na vifungu vya 130(1)(2)(a) pamoja na kifungu
cha 131(1) cha Kanuni ya Adhabu sura ya 16 ya sheria marejeo ya mwaka 2022.
Mshtakiwa alifikishwa Mahakamani kwa mara ya kwanza
tarehe 14.08.2024 na kusomewa shtaka hilo ambalo alilikana na kesi hiyo
kuahirishwa hadi tarehe 21.08.2024 kwa ajili ya kusomwa hoja za awali.
Baada ya Mahakama kusikiliza mashahidi watano (5) wa
Jamhuri akiwemo Mganga aliyemfanyia uchunguzi binti huyo, Mahakama
ilijiridhisha bila ya kuacha shaka kwamba mtuhumiwa alitenda kosa hilo.
Aidha, Mahakama hiyo ilielezwa kuwa mtuhumiwa alitenda
kosa hilo kwa kumvizia binti huyo wakati amekwenda kuchota maji na kumkamata
kwa nguvu kwa kumtishia kummchoma kwa kisu na kisha kumchania nguo zake za
ndani.
Baada ya kutiwa hatiani mshtakiwa aliiomba Mahakama
imuachilie huru kwa kuwa ni mkosaji wa mara ya kwanza kakini mwendesha mashtaka
aliisisitiza Mahakama kumpa adhabu kali mshtakiwa kwa sababu watu wa namna yake
ni hatari kwenye jamii na wamekuwa wakididimiza na kukatiza maendeleo ya
mabinti wenye ndoto za mafanikio.
Licha ya shufaa hizo za mshtakiwa, Hakimu Jagadi
alimuhukumu mshtakiwa kutumikia kifungo cha miaka 30 gerezani.
0 Maoni