WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya
Utamaduni Sanaa na Michezo kuhakikisha inaendelea kushirikiana na wadau
mbalimbali ili kuwawezesha mabondia kunufaika na vipaji vyao.
Ametoa Wito huo jana usiku Desemba 26, 2024, wakati wa
tukio maalum la pambano la ngumi la ‘Knockout ya Mama’ linalofanyika katika
ukumbi wa Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam.
“Awali michezo hii ilikuwa ni ridhaa, lakini kwasasa
tumeweka sheria ambazo zinataka mchezo huu uwe wa kulipwa, ambayo mchezaji
akiitwa na kuweka mikataba ni lazima apate maslahi.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ameitaka Wizara hiyo kwa
kushirikiana na wadau wa mchezo wa ngumi kuendelea kuhakikisha wanatoa mafunzo
bora kwa makocha na wachezaji. “Hii itawezesha kuwa na uhakika kwamba mabondia
wa Kitanzania wanapata ujuzi wa kisasa na wanaendelea kufanya vizuri zaidi.”
Katika Hatua Nyingine, Waziri Mkuu ameitaka Wizara hiyo
kushirikiana na wadau wa mchezo wa ngumi, wahakikishe wanawake wanapatiwa fursa
zaidi ili waweze kushiriki na kuonesha vipaji vyao kwenye michezo hii ya ngumi.
Halikadhalika Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema kuwa Sekta
ya Michezo imefanyiwa maboresho makubwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo
imewawezesha Watanzania kushiriki kikamilifu katika michezo mbalimbali.
Akizungumza kuhusu tukio hilo la Knockout ya Mama,
Mheshimiwa Majaliwa amesema kufanyika kwa tukio hilo kunatokana na kazi kubwa na ushirikiano wa wadau
mbalimbali wenye nia ya kusaidia maendeleo ya jamii hasa mchezo wa ngumi.
Naye, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof.
Palamagamba Kabudi amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mchango mkubwa
ambao ameendelea kuutoa katika sekta ya michezo. “Utashi mkubwa wa Kisiasa wa
Mheshimiwa Rais umeleta msukumo chanya na kuongeza ari na kuchochea ukuaji wa
sekta hii.”
Katika tukio hilo Rais, Dkt. Samia alipiga simu na
kuzungumza na Wadau na mashabiki wa mchezo wa ngumi na kuahidi kuwa Serikali
itaendelea kuweka mikakati ya kukuza sekta hiyo “Najua wapo mabondia wa nje, sasa
Watanzania ibebeni bendera ya Tanzania.”
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akishuhudia mpambano kati ya Mtanzania Mchanza Yusuph na Mphiliponi Miel Fajardo, Katika pambano hilo Yusuph alimshinda.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipokea kutoka kwa Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Palamagamba Kabudi tuzo ya kutambua
mchango wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
katika kuwezesha tasnia ya mchezo wa ngumi nchini, kwenye tukio maalum la
pambano la ngumi la ‘Knockout ya Mama’ linalofanyika katika ukumbi wa Super
Dome, Masaki jijini Dar es Salaam, Desemba 26, 2024.
0 Maoni