Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema umefika wakati kwa
Serikali na taasisi na Mashirika kutambua, kuthamini na kutumia tafiti za
wanasayansi wa ndani ya nchi ili kutatua changamoto zilizopo.
DKt. Biteko
amemsema hayo leo Disemba 2, 2024 wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kufungua Kongamano la tisa
la Sayansi, Teknolojia, Ubunifu na maonesho linaloendelea Jijini Dar es Salaam.
Amesema
wanasayansi nchini wanafanya kazi nzuri na kubwa ya kutafuta suluhu ya matatizo
mbalimbali katika jamii lakini kazi zao zinatambuliwa zaidi nje ya nchi kuliko
zinavyotambuliwa nchini jambo ambalo linaweza kuwavunja moyo.
“Kongamano
hilo ni la kujadili na kutafuta suluhu ya matatizo tuliyonayo, tutumie tafiti
za wanasayansi wa ndani badala ya kuwavunja moyo na kila anayejaribu kwa
kutafiti apewe fursa ili aendelee kutafiti zaidi na matokeo tutayaona,” amesema
DKt. Biteko.
Ameongeza
kuwa Serikali inatambua mchango wa wanasayansi na kuwawezesha watafiti na
wabunifu na kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia COSTECH imetoa kiasi cha
bilioni 32 kwa ajili ya kuimarisha miradi ya utafiti na ubunifu.
Tangu mwaka
2015 Serikali imeshapokea kiasi cha shilingi bilioni 222.8 kwa ajili ya kujenga
uwezo kwa wanasayansi wabunifu kuendeleza miradi mbalimbali ambazo zimesaidia
kuwajengea uwezo wanasayansi wakiwemo wanasayansi vijana.
Naye Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia. Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali imeanza
kutambua jitihada za Wanasayansi, Watafiti wa ndani ya nchi na baadhi yao
wametunukiwa vyeti kwa kutambua mchango wao kwa maendeleo yaliyofikiwa katika
sekta mbalimbali ikiwemo Afya, Kilimo na Uvuvi.
Amefafanua
kuwa njia moja yakufanya jitihada hizo kuwa endelevu, Serikali imeanzisha mfuko
wa mikopo nafuu wa kubiasharisha bunifu na tafiti Tanzania unaojulikana kama
Samia Fund.
Kwa upande
wake, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu ameishukuru Serikali kwa
uwezeshaji ambao umeiwezesha kutekeleza majukumu yake kwa viwango na kuwa moja
ya taasisi mahiri ya kupigiwa mfano Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Ameongeza
kuwa COSTECH kupitia program mbalimbali imewasaidia vijana wengi kubadili ndoto
zao kuwa fursa ambapo pamoja na mambo mengine imefikia uwezo wa kutoa vibali
1000 kwa watafiti kutoka nje ya nchi.
Balozi wa
Norway nchini, Mhe. Tine Tonnes ameipongeza Tanzania kufuatia hatua zake za
kuendeleza watafiti na wabunifu huku akieleza utayari wa nchi hiyo kuendelea
kuunga mkono program za uhifadhi wa mazingira.
Vikundi 19
vimepokea mfano wa hundi ya Shilingi Bilioni 6.3 ikiwa ni mkopo kwa watafiti,
wabunifu waliofanya kazi inayosababisha matokeo.


0 Maoni