Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Innocent Bashungwa
amefika eneo ilipotokea ajali ya basi la abiria lenye namba za usajili T857
DHW, katika eneo la Kabukome katika Kata ya Nyarubango wilayani Biharamulo
mkoani Kagera na kuwajulia hali majeruhi wanaoendelea kupewa matibabu katika
hospitali teule ya Biharamulo, tarehe 21 Desemba 2024.
Basi hilo liliokuwa linafanya safari kutoka Kigoma kwenda
Bukoba wakati liliposimama kushusha abiria ambae alipitilizwa kwenye kituo,
lilishindwa kuondoka na kuanza kurudi nyuma kisha kuacha njia na kupinduka.
Ajali hiyo imesababisha vifo vya abiria 11 na majeruhi 16
ambapo majeruhi wanaendelea na matibabu katika hospitali teule ya Biharamulo
mkoani Kagera.
Akizungumza baada ya kutembelea majeruhi, Waziri
Bashungwa ametoa pole kwa familia, ndugu na jamaa wote walioguswa na ajali hiyo
na kutoa wito kwa Watanzania kuendelea kuwaombea majeruhi wapone haraka.
“Nitumie nafasi hii kuombea raho za marehemu ambao
tumewapoteza katika ajali ambayo imetokea hapa Biharamulo, tumepoteza ndugu
zetu 11, wametangulia mbele za haki,” amesema Bashungwa.
Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa Wizara imeanza kufanyia
kazi Maelekezo ya Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanya marekebisho
ya kuwa na mfumo wa leseni za udereva ili kuwapunguzia alama madereva wanafanya
makosa yenye kuhatarisha usalama barabarani ambazo zitapelekea kuwafungia
leseni.
Kwa Upande wake, Mganga Mkuu wa Hospitali teule ya
Biharamulo, Gresmus Sebuyoya ameeleza kwa majeruhi 26 wameruhusiwa na wengine
16 wanaendelea na matibabu na ungalizi wa karibu.
“Tumebaki na watoto wanne ambao wanaendelea vizuri,
wanaume tunao sita, vifo tulikuwa navyo kumi na moja, wanawake watano, wanaume
wanne na watoto wawili,” ameeleza
Daktali Gresmus.
0 Maoni