Waziri wa
Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Jerry Silaa amewataka waandishi wa
habari kuzingatia kanuni, sheria na maadili ya uandishi wa habari wakati
wakiripoti habari za uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na Uchaguzi Mkuu
utakaofanyika mwakani.
Mh. Silaa
ametoa kauli hiyo leo Jijini Dar es Salaam katika Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Habari Kuelekea
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025 uliohudhuriwa pia na
Makamanda wa Jeshi la Polisi wa mikoa yote nchini.
Mhe. Silaa
amesema kwamba vyombo vya habari vinawajibu wa kuwahabarisha wananchi kuhusiana
na uchaguzi kwa kuhakikisha kuwa vinatenda haki ya kutoa habari za uhakika na
zilizochakatwa kwa weledi mkubwa.
Amesema kuwa
wizara yake inatambua mchango unaotolewa na vyombo vya habari kwa kutoa habari
mbalimbali za miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali, na kuahidi kuwa yeye
yupo tayari kutoa ushirikiano wa kutosha kwa vyombo vya habari.
Mhe. Silaa
ameeleza kuwa kutokana na kuboreshwa kwa mazingira rafiki ya vyombo vya habari
nchini hadi sasa, Tanzania ina jumla ya magazeti 179, Majarida 174, Radio 247,
Mitandaoni 355 pamoja na Runinga 68 zilizosajiliwa.
Kwa upande
wake Msemaji wa Jeshi la Polisi David Misiime amesema kuwa kuna umuhimu wa
vyombo vya habari kufanya kazi kwa ushirikiano katika matukio mbalimbali
yakiwemo ya uchaguzi ili kuepusha migongano wakati wa kutekeleza majukumu yao.
“Ni muhimu
polisi kutambua na kuheshimu mipaka ya kitaaluma ya waandishi wa habari na
vivyo hivyo kwa waandishi wa habari kuheshimu mipaka ya kitaaluma ya polisi wakati
wakitekeleza majukumu yao,” alisema Kamanda Misiime.

0 Maoni