Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko amemwakilisha Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Phillip Mpango kufungua
mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Mashirika ya Umma nchini SHIMMUTA na
kuagiza mashirika kuondokana na visingizio visivyo na msingi ili kutimiza azma
ya mashindano hayo.
Dkt. Biteko
ametoa maelekezo hayo Jijini Tanga ambapo amesema kumekuwa na visingizio vya
kuwakosesha watumishi wa umma kushiriki mashindano ilhali ni suala
linalofahamika na liko kwenye kalenda ya kila mwaka ya mashirika husika.
“Utaratibu
huu wa kukubaliana jambo lakini jambo tulilokubaliana halifanyiki inatufanya
tukose uhalali wa kuwasimamia wengine, nilitaka kujua kwanini hatupeleki
washiriki katika mashindano haya. Kama tunaona mashindano haya sio ya muhimu ni
bora tuondokane nayo tufanye jambo linguine,”amesema Dkt. Biteko.
Amewataka
viongozi wa SHIMMUTA kuwatembelea waajiri na kuwahimiza waajiri kuwaruhusu
watumishi kushiriki katika mashindano hayo, “hakuna jambo linalouma kwamba
baadhi ya watumishi wengine wanashiriki na wengine wanapewa visingizio jambo
ambalo halikubaliki kwa namna yoyote na sio sawa,”amesisitiza Dkt. Biteko.
Amesema
SHIMMUTA haina sababu ya kujipongeza kwa kuvunja rekodi ya kupata washiriki
ilhali yapo mashirika mengi ambayo viongozi wake hawajatuma washiriki katika
mashindano hayo huku akitoa mfano kuwa kujipongeza kwa hatua hiyo ni sawa na
kushangilia goli la kujifunga.
Amefafanua
kuwa kutekeleza maelekezo ya serikali kuhusu kushiriki katika michezo kutapunguza
gharama na kuwaepusha watumishi na magonjwa yasiyo ya kuambukiza sambamba na
kuongeza tija na ufanisi kazini.
Awali, Mkuu
wa Mkoa wa Tanga, Balozi, Dkt. Batilda Burian amewapongeza washiriki na
waandaaji wa mashindano hayo na kuwahakishia utayari wa mkoa kuendelea
kuboresha mazingira kwa ajili ya kuwezesha ushiriki mzuri zaidi.
Kwa upande
wake Mwenyekiti wa SHIMMUTA Taifa, Roselyne Massam ameishukuru serikali kwa
kutoa fursa inayowawezesha watumishi kushiriki michezo na hivyo kuwa nyenzo ya
kuongeza mshikamano miongoni mwa watumishi kwa ujumla.
Ameiomba
Serikali kuwezesha ukamilishaji wa sera ya taifa ya michezo ya SHIMMUTA ili
kuweka msingi wa ushiriki na umuhimu wa mashindano hayo kwa watumishi.
Jumla ya
watumishi 4720 kutoka mashirika ya umma 96 wanashiriki mashindano hayo
yanayoendelea Jijini TANGA.


0 Maoni