WAZIRI wa
Madini, Mheshimiwa, Anthony Mavunde amewataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa
kuendelea kusimamia sheria kwenye utendaji kazi ili kuepuka migogoro inayoweza
kujitokeza kati ya wachimbaji wa madini na ajali kwenye shughuli za uchimbaji
na uchenjuaji wa madini.
Waziri
Mavunde ametoa rai hiyo kwenye kikao kazi cha menejimenti ya Tume ya Madini
kilichofanyika mapema leo Novemba 18, 2024 chenye lengo la kuweka mikakati ya
kuendelea kuimarisha Sekta ya Madini kuanzia kwenye ukusanyaji wa maduhuli,
usimamizi wa sheria, biashara ya madini na mchango wake kuendelea kukua kwenye
Pato la Taifa.
Amesema kuwa
kuendelea kusimamia sheria katika utendaji kazi kumewasaidia Maafisa Madini
Wakazi wa Mikoa wengi kuwepo hapa leo hii.
Katika hatua
nyingine amepongeza kasi ya ukusanyaji wa maduhuli inayofanywa na Maafisa Madini
Wakazi wa Mikoa na kuwataka kuendelea kuwa wabunifu hasa kwenye udhibiti wa
mianya ya upotevu wa mapato.
Wakati
huohuo Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amewaagiza
wakaguzi migodi kufanya ukaguzi wa mara
kwa mara kwenye migodi hususan kipindi hiki cha mvua ili kuepusha majanga
migodini.
“Kuanzia
kipindi hiki mpaka Aprili mwakani ni kipindi cha mvua, mfanye ukaguzi mara kwa
mara, migodi isiyoridhisha ifungiwe hadi itakapoboreshwa, hatutavumilia vifo
vya uzembe migodini,”amesema Mhandisi Samamba.
Naye, Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo amewataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kutimiza majukumu yao sio tu kufikia lengo la Shilingi Trilioni moja, malengo yapo mengi na
makubwa na kwamba sekta ya madini inatakiwa kuchangia kwenye pato la Taifa
kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.
“Tufanye
udhibiti wa kutosha, tukasimamie sheria, kanuni na taratibu tutafikia mchango
wa asilimia 10 na kuzidi,”amesisitiza Mbibo.
Katika hatua
nyingine, Mbibo ameelekeza Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuangalia namna bora
ya kudhibiti mianya ya utoroshaji wa madini hasa kwenye maeneo ya mipakani na
viwanja vya ndege.



0 Maoni