Wananchi wafurahia ujenzi wa barabara ya Malichewe, Sumbawanga

 

WANANCHI wa Kata ya Kizwite, Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa wameishukuru Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kurahisisha mawasiliano ya barabara ya Malichewe na kuwapunguzia changamoto ya kutembea umbali mrefu kutoka kata hiyo kwenda Sumbawanga Mjini.

Mhe. Andrea Barnaba Diwani wa Kata ya Kizwite, ameishukuru serikali kwa kuwajengea barabara hiyo kwani hapo awali kulikuwa na mashimo na makorongo makubwa ambapo magari na bajaji yalikuwa yanapita kwa shida na kusababisha wananchi kupandishiwa nauli kufika mjini.

“Tunaishukuru serikali kwa kutuletea barabara ya lami, hapo awali wananchi walilazimika kufanya mzunguko mkubwa na kutumia gharama kwenda mjini, walikuwa wanalipa nauli shilingi 1000 lakini sasa hivi wanalipa shilingi 500 kufika mjini kufuata huduma mbalimbali," alisema.

Naye, mkazi wa Mtaa wa Mkumbuke, Bi. Veronica Mwanyeche amesema, zamani kipindi cha mvua barabara hiyo ilikuwa haipitiki kutokana na kujaa matope sasa hivi wanafika mjini kwa urahisi na huduma nyingi zimewafikia huku wengine wakijenga nyumba za kisasa kutokana na uwepo wa barabara nzuri.

Bw. Florence January mkazi wa Kizwite Sokoni, anayejihusisha na kutoa huduma za kusafirisha abiria amesema, hapo awali alikuwa anapata shida kusafirisha abiria kwa sababu ya vumbi na matope hata hivyo baada ya matengenezo hayo hajapata changamoto yoyote huku akiipongeza serikali kwa kuwajali wananchi wake.

Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Wilaya ya Sumbawanga, Mhandisi Dickson Kanyankole amesema mradi wa barabara ya Malichewe yenye urefu wa Kilomita 1.2 umejengwa kwa kiwango cha lami kwa thamani ya shilingi milioni 871 ambapo mradi umekamilika na wananchi wanasafiri bila shida.

Ameongeza kuwa kwa sasa wanajenga mita 800 na kipande kinachobakia mita 400 kitajengwa mwaka wa fedha 2025/26 ili kukamilisha barabara nzima yenye Km 2.4 kwa kiwango cha lami.

Hata hivyo, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutunza na kuilinda miundombinu ya barabara kwa kufanya usafi wa mitaro kwani ni wajibu wao kuitunza ili waendelee kunifaika nayo kwa muda mrefu.

Chapisha Maoni

0 Maoni