Umoja wa Waigizaji Mkoa wa Dar es
Salaam wapongezwa kwa kubeba maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutangaza utalii.
Maneno haya yamesemwa jana Novemba 2,
2024 na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Saad Mtambule katika tamasha la
"Shtuka, boresha afya ya akili ndani ya Hifadhi ya Pande"
lililoandaliwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa
kushirikiana na Umoja wa Waigizaji Mkoa wa Dar es Salam.
"Niwapongeze wasanii wa sekta ya
uigizaji kwa kubeba maono ya Rais Samia ya kuitangaza sekta ya utalii na hasa,
Hifadhi yetu ya Pande ambayo inapatikana kwenye Wilaya yetu ya Kinondoni,"
amesema Mhe. Mtambule.
"Pia tuendelee kutumia akaunti
zetu za mitandao ya kijamii kuhamasisha makundi mbalimbali ili yaweze kuja
kutembelea hifadhi ya Pande," aliongeza Mhe. Mtambule.
Vilevile, Mhe. Mtambule, aliwashukuru
wasanii kwa kutembelea hifadhi hiyo na alisisitiza kuwa utangazaji wa shughuli
za utalii ukiongezeka wageni watafurika na hivyo uchumi wa Nchi utakua.
Kadhalika, Mhe. Mtambule ameipongeza
TAWA kwa jitihada zake katika kuboresha hifadhi ya Pande kwa kuongeza mazao
mbalimbali ya utalii ikiwemo uanzishwaji wa bustani ya wanyamapori mbalimbali
wakiwemo Simba, Duma, Chatu, Mamba, Nyumbu, Pundamilia nk.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi
Mwandamizi, William Kitebi akimuwakilisha Kamishna wa Uhifadhi TAWA, alitoa
shukrani zake za dhati kwa Mhe. Mtambule kwa ushirikiano wake na TAWA katika
masuala ya uhifadhi wa hifadhi za Pande na Kunduchi. Vilevile aliwashukuru
Umoja wa waigizaji Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuja kutembelea hifadhi ya Pande.
Naye, Mwenyekiti wa Umoja wa waigizaji
Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Leonard Mwinuka amesema wao kama wasanii wataendelea
kumuunga mkono Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika utangazaji wa utalii. Pia
aliishukuru uongozi wa TAWA kupitia Hifadhi ya Pande kwa kuwapa ushirikiano wa
kutosha, " Mbegu mliyopanda kwetu, itaota na tutakuwa mabalozi wazuri wa
kuelezea uzuri wa hifadhi hii," alisisitiza, Bw. Mwinuka.
Tamasha hili lilihudhuriwa pia na
viongozi mbalimbali wa TAWA pamoja na Bodi ya Utalii Tanzania ( TTB) wakiwemo
Kamishna Msaidizi Mwandamizi anayeshughulikia huduma za biashara, Hamza
Hassani, Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Sylvester Mushy, Mkurugenzi
wa Masoko kutoka TTB, Ernest Mwamaja pamoja na Kamanda wa Pori la Akiba Pande,
Dorothea Massawe.
Sambamba na hilo, tamasha hili
liliambatana na zoezi la uchangiaji wa damu salama.
Na. Joyce Ndunguru, Dar es Salaam

0 Maoni