Wanawake zaidi ya 30 kutoka mikoa
mitatu ya Dodoma, Morogoro na Dar es Salaam wameamua kumuunga mkono Rais Samia
Suluhu Hassan kwa kutangaza vivutio vya utalii nchini baada ya kutembea umbali
wa zaidi ya kilometa nne kupanda mlima Sanje kutembelea Maporomoko ya maji
Hifadhi ya Taifa ya Milima Udzungwa.
Zoezi hilo lilifanyika jana
lilimhusisha pia mama mwenye mtoto wa umri wa miezi sita Agnes Samweli, ambapo
baada ya kufika kwenye maporomoko alisema amekuwa akisikia kwa muda mrefu
Hifadhi hiyo hivyo alipopata fursa aliamua kuja na mwanae kuitembelea.
Agnes alisema kuwa alipomsikia Rais
Samia akitangaza vitutio vya utalii vilivyopo hapa nchini alihamasika kwenda
kutalii na kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Milima Udzungwa kuona maajabu ya
Mungu ya maporokoko ya maji.
“Wakati mama Samia anatangaza vivuto
vilivyopo nchini nilikuwa mjamzito na baada ya kujifungua mwanangu wa kike
akiwa na miezi sita nimepata fursa ya kuja sikutaka kuiachia na ndiyo sababu
nimekuja na mwanangu kutalii hapa Hifadhi ya Taifa ya Milima Udzungwa ili
kutembelea maporomoko ya maji,” alisema Agnes.
Naye Dk Sarah Mwafalo,alisema
ametembela Hifadhi ya Taifa ya Milima Udzungwa na kwamba amejifunza mambo mengi
ya utalii na kwamba mbali na kutembelea maporomoko pia kitendo cha kutembea kwa
miguu umbali wa kilometa zaidi ya nne ni
mazoezi muhimu kwa afya ya binadamu.
Sarah alisema kwamba wanawake wote
waliotembelea Hifadhi hiyo mbali na kufanya utalii wa ndani pia wanafanya
mazoezi na hivyo wameweza kuimarisha afya zao kwa ujumla hususani ya akili na
pale watakaporudi kwenye majukumu yao watafanya kazi zao kwa ufasaha zaidi.
Kwa upande wake Elizabeth Tarimo mkazi
wa Dodoma alisema kuwa ametumia usafiri wa Reli ya Mwendo kasi kutoka Dodoma
kuja Morogoro kwa ajili ya kutalii Hifadhi ya Taifa ya Milima Udzungwa ambapo
aliishukuru serikali kwa ujenzi wa reli hiyo na aliwataka wananchi kutumia
fursa hiyo kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo mkoani Morogoro ikiwemo
Hifadhi ya Taifa Mikumi.
“Watanzania tuna kila sababu ya
kujivunia usafiri huu wa SGR hivyo natumia fursa hii kuwahamisisha wananchi
wenzangu kutumia Reli ya Mwendo kasi kuja Morogoro kufanya utalii wa ndani kwa
kutembelea vivutio vilivyopo nchini hususani mkoa wa Morogoro.”
Naye Afisa Uhifadhi, Kitengo cha
Utalii,Hifadhi ya Taifa ya Milima Udzungwa, Ahmed Nassoro alisema Hifidhi hiyo
ni maarufu nchini kutokana na kuwa na viumbe adimu kama Mbega mwekundu wa
Udzungwa,Ng’olaga wa Sanje,jamii za Ndege kama Chozi Mbawa Nyekundu na Kware wa
Milima ya Udzungwa kuliko maeneo mengine yote na kwamba watalii wa ndani na nje
wanaotembelea hifadhi hiyo huvutiwa na vivutio vyote vinavyopatikana hapo.
Ahmed Nassoro aliwataka Watanzania wote
kuendelea kutembelea Hifadhi hiyo kwani kitendo cha kuona vivutio vinavyopatika
katika Hifadhi ya Taifa ya Milima Udzungwa kutawafanya kuimarisha afya ya akili
na pia kutawasaidia kujiepusha na magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza kwani ili
ufike eneo husika mtu hulazimika kutembea kwa miguu kitendo kinachojenga mwili
kwa mazoezi.
Hifadhi ya Taifa ya Milima Udzungwa ni
miongoni mwa Hifadhi za Taifa maarufu kwakuwa na viumbe adimu duniani na
maporomoko ya maji hivyo watalii wengi hutembelea Hifadhi ya Milima
Udzugwa na kuchangia ongezeko la pato la Taifa.
Na. Zainabu Ally- Udzungwa


0 Maoni