Diwani wa Kata ya Mkiwa Mhe. Stephen
Petro Mtyana amesema kambi iliyowekwa na Askari wa TAWA katika Kijiji cha Mkiwa
kilichopo Kata ya Mkiwa wilaya ya Ikungi Mkoani Singida yenye lengo la
kuwafukuza tembo imerejesha amani na matumaini kwa wananchi wa Kijiji hicho
ambao wamekuwa wakisumbuliwa na wanyamapori hao kwa muda mrefu.
Mhe. Stephen Mtyana ameyasema hayo jana Novemba 02, 2024 alipokuwa akiongea na waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya
habari katika Kijiji cha Mkiwa baada ya kutembelea Kambi hiyo ya Askari.
"Wanyama hawa wamekuwa wasumbufu,
siku hadi siku kuanzia huko nyuma lakini kwasasa baada ya kufika kikosi hiki
cha wataalamu kutoka TAWA wametusaidia kuwaondoa hapa walipo kwenye makazi yetu
na kuwapeleka mbali," amesema Mhe. Stephen.
"Bahati nzuri wametuletea ndege
nyuki wanaoweza kuwafukuza tembo na kuwapeleka mbali zaidi, sambamba na hilo
basi sina shaka na Askari wa TAWA ambao tangu wamefika tembo wamekuwa mbali na
maeneo yetu na hii inatupa picha halisi kwamba Mhe. Rais Dkt .Samia Suluhu Hassan anawajali watu wake
ili waweze kukaa salama salimini" ameongeza na kusisitiza Diwani huyo.”
Naye Afisa Habari wa TAWA Beatus
Maganja amesema kufuatia changamoto ya wanyamapori hao, Wizara ya Maliasili na
Utalii kupitia TAWA imeona umuhimu wa kuweka Kambi katika Kijiji cha Mkiwa ili
kuhakikisha maisha na mali za wananchi wa Kijiji hicho vinakuwa salama.
Aidha amesema TAWA imepeleka vikosi vitatu
vya Askari zaidi ya 20 vikiwa na vitendea kazi vya kutosha kukabiliana na
wanyamaporihao ikiwemo magari matatu, silaha za moto, na ndege nyuki mbili ikiwemo
ndege nyuki kubwa aina ya DJI Agras T30
yenye uwezo wa kubeba Lita 10 za maji yenye pilipili maalumu Kwa ajili
ya kuwafukuza tembo.
Maganja ameomba ushirikiano kutoka Kwa
wananchi wa Kijiji hicho na kuwataka kuondoa wasiwasi kwakuwa Askari wa TAWA
wamejipanga na wako timamu Kwa ajili ya kuwakabili wanyamapori hao.
Kwa upande wake Afisa Uhifadhi kutoka
Kanda ya Kati ya TAWA Winnie Kweka amesema awali Mamlaka imekuwa ikifanya
jitihada mbalimbali zenye lengo la
kuwasaidia wananchi wa wilaya hiyo ikiwemo kuwapa elimu na mbinu za kujilinda
dhidi ya athari ya wanyamapori hao.
Aidha amebainisha kuwa Kijiji hicho na
wilaya ya Ikungi kwa ujumla pamoja na
maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Singida
yameangukia katika mfumo ikolojia wa Ruaha - Rungwa, mfumo unaotajwa
kuwa na tembo wengi ambao wamekuwa wakipita katika Kijiji cha Ukiwa na kuelekea
Pori la Akiba Swagaswaga Kwa ajili ya
kupata mahitaji yao ya msingi.
Kutokana na hali hiyo Mhifadhi Winnie
Kweka ametoa wito kwa wananchi hao kuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi na
kuepuka kufanya shughuli zao kwenye shoroba.




0 Maoni