Mjumbe wa
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa ambaye pia ni
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema katika
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa mwaka 2024, CCM imedhamiria kuendelea
kutekeleza miradi ya maendeleo ili kubadilisha hali za maisha ya wananchi.
Amesema Kata
ya Namonge ni kati ya kata 17 za Wilaya ya Bukombe yenye vijiji vinane na
vitongoji 36 ambayo imeendelea kupiga hatua ya maendeleo kwa kuwa na mtandao
mrefu zaidi wa barabara kuliko kata zingine.
Dkt. Biteko
amesema hayo leo Novemba 25, 2024 wakati akihutubia katika Kampeni za Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa wilayani Bukombe zilizofanyika katika Uwanja wa Shule ya
Msingi Namonge mkoani Geita.
“Tunataka
maendeleo kwa ajili ya watu wetu na kata hii imeandikisha idadi kubwa ya
wananchi leo nimekuja kuwaomba mchague viongozi wa CCM ili tuendeleze jitihada
zetu za kuwaletea maendeleo,” amesema Dkt. Biteko.
Ametaja
miradi ya maendeleo iliyotekelezwa katika kata hiyo kuwa ni ujenzi wa shule za
tatu za sekondari, zahanati nne na kituo cha afya kimoja.
“Awali
tulikuwa na barabara kutoka Uyovu hadi Namonge na barabara ya kwenda maeneo
mengine haikuwa nzuri, barabara ya kutoka Namonge hadi Mjimwema haikuwepo.
Hatua iliyopigwa ni kubwa na leo tumekuja na kazi moja ya kuomba kura zenu
wananchi wa Namonge,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Amebainisha
mipango ya maendeleo ya baadae kuwa ni kujenga shule ya sekondari na kuimarisha
hospitali ili iweze kutoa huduma za upasuaji katika kata hiyo.
Ameendelea
kusema ili kufanya kazi vizuri zaidi ni vyema kupata viongozi wa vijiji na
vitongoji wanaotokana na chama kimoja kwa vile wanauhusiano mzuri wa kazi na
hivyo kurahisisha juhudi za kuleta maendeleo kwa wananchi.
Pamoja na
hayo, Dkt. Biteko amewahimiza wananchi wa Bukombe na Watanzania wote kwa ujumla kujitokeza kwa wingi na kupiga
kura ili kuchagua viongozi wao.
“Tunatambua
uchaguzi huu ni muhimu na sisi tunausimamia kwa haki ili kupata viongozi
watakaotatua shida za wananchi,” amebainisha Dkt. Biteko.
Naye,
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Bukombe, Matondo Lutonja amesema
itakapofika siku ya kupiga kura Novemba 27, 2024 wananchi wa Bukombe wajitokeze
kwa wingi ili kutimiza haki yao ya kikatiba.
Kampeni za
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa nchini zitahitimishwa Novemba 26, 2024 na mkoani
Geita kampeni hizo zitafanyika Kata ya Runzewe Magharibi ambapo Dkt. Biteko
atakuwa mgeni rasmi.
0 Maoni