Serikali
kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imekuwa ikifanya
jitihada mwaka hadi mwaka za kuimarisha na kuboresha miundombinu ya barabara
ili kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kuzilinda ziweze kutumika
kwa muda mrefu.
Meneja wa
TARURA Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Chacha Moseti amesema, Serikali ya Awamu ya Sita
inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan
imefanya kazi kubwa katika kuimarisha mtandao wa barabara ili uweze kupitika
kwa misimu yote kwa kutenga fedha mwaka hadi mwaka.
“Tunamshukuru
Rais Samia kwa kuongeza bajeti ya TARURA Mkoa wa Rukwa kutoka shilingi Bilioni
5.1 hadi kufikia shilingi Bilioni 12.9, kwa kiasi kikubwa imesaidia kuimarisha
mtandao wa barabara katika mkoa wetu,” amesema.
“Kupitia
ongezeko hilo TARURA mkoa wa Rukwa, inaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati
kwa kufungua barabara mpya ili kufika kusiko fikika na kuboresha barabara
zilizopo ili zipitike wakati wote,” ameongeza.
Amesema,
barabara za lami zimeongezeka kutoka Km 29.33 na kufikia Km 43.14 ambazo ni
sawa na ongezeko la Km 13.81%, wamejenga barabara za zege Km 0.631, barabara za
changarawe Km 480.76 na ujenzi wa madaraja na maboksi kalavati 147.
Ameeleza,
wameweza kuongeza idadi ya madaraja na kufungua maeneo yaliyokuwa hayafikiki na
sasa yanafikika muda wote kwa kujenga madaraja 17 kwa kutumia teknolojia ya
mawe katika Halmashauri za Wilaya ya Sumbawanga, Kalambo na Nkasi.
Ameongeza
kuwa, wametekeleza miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa daraja la mto Kalambo
lenye urefu wa mita 80 ambalo limenufaisha wananchi wa kata za Sopa na Pombwe
wilayani Kalambo kusafirisha mazao yao sokoni kwa urahisi.
Mkazi wa
Nkasi Bi. Sarafina Mbalamwezi, ameipongeza serikali kwa kile inachokifanya
kuhakikisha miradi ya barabara inatekelezwa na kukamilika kwa wakati na
wananchi kuondokana na changamoto ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma
mbalimbali ikiwemo ya matibabu.
Mkazi wa
Sopa wilayani Kalambo, Bw. Amon Kabwe amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
kwa kazi kubwa ya kuboresha miundombinu vijijini ili kuhakikisha wananchi
wanasafiri na kusafirisha mazao yao sokoni kwa urahisi.
TARURA Mkoa
wa Rukwa inahudumia mtandao wa barabara wenye urefu wa Kilomita 2,304.26 ambapo
kati ya hizo barabara za lami ni Km 44.3, barabara za changarawe Km 1,145.68 na
barabara za udongo Km 1,114.28.


0 Maoni