Mjumbe wa
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa ambaye pia ni
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka
wananchi wa Nyamongo na Mkoa wa Mara kwa
ujumla kufanya kampeni za kistaarabu na kujitokeza kupiga kura katika Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba
27, 2024.
Dkt. Biteko
ameeleza kuwa maendeleo hayaletwi kwa matusi wala kuvunjiana heshima na kuwa
wananchi hao washinde ubaya kwa wema. Aidha, Dkt. Biteko amefika eneo hilo kwa lengo la kuwaomba wananchi wa
Nyamongo wachague watu ambao wataungana na Serikali katika kuwaletea maendeleo.
Dkt. Biteko ameyasema
hayo leo Novemba 20, 2024 wakati akifungua kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Mkoa wa
Mara zilizofanyika katika Mji wa
Nyamongo Wilaya ya Tarime.
“Mwaka huu
tuna Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni uchaguzi mkubwa wa kumchagua mtu
atakayejua hali na maisha ya watu katika ngazi ya mtaa na ambaye atabeba shida
za watu na kuzitatua,” amesema Dkt. Biteko.
Amebainisha
kuwa uchaguzi huo ni muhimu na sio wa majaribio hivyo ni lazima wananchi
wachague viongozi ambao sio walalamikaji na kuwa maendeleo hayaletwi kwa
matusi bali kwa kufanyakazi.
“CCM
tumekuja hapa kuwaomba kura zenu si tu
kwa sababu huu ni msimu wa kuomba kura umefika ila kazi tunaweza kuifanya,
tumeshaifanya na tuna cha kuonesha, mtakumbuka mwaka 2020 tulikuja na ilani na
kusema tutakayoyafanya na tumeeleza hapa tuliyoyafanya,” amesisitiza Dkt.
Biteko.
Amesema kuwa
licha ya kufanya siasa ni lazima viongozi wajue wajibu wao ni kuwaletea
wananchi maendeleo akitolea mfano namna kijiji cha Nyamongo kilivyolipwa shilingi
bilioni nne ikiwa ni fidia kwa wananchi.
Amefafanua
kuwa Rais Samia ana dhamira ya dhati ya kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo
na kuwa na maisha nafuu hivyo wananchi wa Nyamongo wamuunge mkono kwa kuchagua
wagombea wa CCM.
Katika hatua
nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa kuna fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi
kwa jamii (CSR) zinazohitaji kibali kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na kuwa amemuelekeza Katibu Mkuu TAMISEMI
kuhakikisha kibali hicho kinatoka kabla ya mwisho wa juma hili ili wananchi wa
eneo hilo waweze kunufaika kwa kupata miradi ya maendeleo.


0 Maoni