Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde
amewakaribisha jumuiya ya wa Wafanyabiashara kutoka Nchini Finland kuwekeza
kwenye sekta ya madini kwa kuwa nchi ya Tanzania imejaaliwa kuwa na rasilimali
ya kutosha ya madini, mazingira ya uwekezaji rafiki na sera zinazotabirika.
Waziri
Mavunde ameyasema hayo jana Masaki
Jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa kifungua kinywa ulioandaliwa na
Ubalozi wa Finland nchini kwa lengo la kuwakutanisha wafanyabiashara wa Madini
kutoka Finland na Wizara ya Madini ili kubaini maeneo ya ushirikiano na fursa
za kiuchumi zilizopo sekta ya madini nchini Tanzania.
Akizungumza
katika hafla hiyo Balozi wa Finland nchini Tanzania Mh. Theresa Zitting amesema
Tanzania na Finland ni nchi zenye ushirikiano mkubwa kwenye masuala ya kiuchumi
na hivyo ni wakatinmuafaka sasa kuimarisha mahusiano hayo kupitia uwekezaji
kwenye sekta ya madini ambapo amepongeza hatua kubwa zinazofanywa na Mh. Rais
Dkt. Samia S. Hassan kukuza sekta ya madini nchini na kuifanya kuwa sekta
muhimu kwenye kuchangia maendeleo ya uchumi ya Tanzania.
Naye
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti Madini ya Finland (GTK) Prof.
Tiilikainen Kimmo amesema kwamba kupitia makubaliano (MoU) kati ya GTK na
Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST), Finland itashirikiana na Serikali
ya Tanzania kuimarisha shughuli za Utafiti wa madini ili kuiwezesha Tanzania
kufikia Dira ya 2030 ya Madini ni 𝐌𝐀𝐈𝐒𝐇𝐀 𝐧𝐚 𝐔𝐓𝐀𝐉𝐈𝐑𝐈 ambapo Tanzania imejipanga kufanya
utafiti wa kina wa madini wa kufikia eneo la 50% la eneo la nchi nzima.
Akiwasilisha
hotuba yake Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde amewakaribisha wafanyabiashara
kutoka Finland kuja kuwekeza nchini Tanzania kwa kuwa Tanzania ina fursa nyingi
za kiuchumi kupitia sekta ya madini na hasa madini mkakati ambayo kwa sasa yana
uhitaji mkubwa Duniani.
“Mh. Rais
Dkt. Samia S. Hassan kupitia Falsafa yake ya uongozi wa 4R ameweka mazingira
rafiki ya biashara na uwezekaji nchini Tanzania na hivyo Tanzania ni sehemu
salama ya kufanya uwekezaji.
Tanzania
imejaaliwa rasilimali madini ya kutosha na hivyo kuifanya nchi yetu kuwa na
nafasi nzuri kuvutia uwekezaji.
“Hivyo
tunafungua milango kwa wafanyabiashara kutoka nchini Finland kuchangamkia fursa
za uwekezaji kupitia sekta ya madini,” alisema Waziri Mavunde.
Wafanyabiashara
hao wapo nchini kuhudhuria mkutano wa Kimataifa wa Madini na Uwekezaji 2024
unaofanyika nchini Tanzania.



0 Maoni