Wakala ya
Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Manyara ina mpango wa kufungua
barabara mpya zenye urefu Km. 109 katika Wilaya ya Mbulu, Simanjiro pamoja na
Babati katika mwaka wa fedha 2024/2025.
Hayo
yamebainishwa na Kaimu Meneja wa TARURA Mkoa wa Manyara Mhandisi Salim Bwaya
wakati akiongea na waandishi wa habari mkoani hapo hivi karibuni.
Mhandisi
Bwaya amesema kwamba kilomita hizo za barabara zinaenda kuwanufaisha wananchi
na kuwaletea manufaa ya kiuchumi na kijamii kwa kuwarahisishia kupata huduma za
kijamii kwa urahisi.
“Mwaka huu
wa fedha tuna mpango wa kufungua barabara katika wilaya ya Mbulu (Km. 46), Simanjiro (Km. 41), pamoja
na Babati (Km. 22) ambapo itajumuisha ujenzi wa barabara za lami(Km.
11.7),changarawe (Km. 251.4) pamoja na matengenezo ya barabara za udongo (Km.
385) na ujenzi wa vivuko vipatavyo 104," amesema.
Amesema
kwamba licha ya kufungua kilomita hizo za barabara hali ya mtandao wa barabara
katika maeneo mengi katika Mkoa huo ni nzuri kwani unapitika katika kipindi
chote cha mwaka.
Aidha,
amesema kuwa utekelezaji huo unaendelea kutokana na ongezeko la bajeti katika
mkoa huo ambapo kwa sasa bajeti yao imepanda mara tatu kutoka Shilingi bilioni
6.788 mwaka 2021 hadi kufikia Shilingi bilioni 19.7 mwaka 2024/2025.
“Hili ni
ongezeko kubwa na limetuwezesha kuongeza ubora wa mtandao wetu wa barabara kwani mwaka 2021 tulikuwa na
barabara za lami Km. 17 na sasa tuna Km. 33.03, barabara za changarawe kutoka
Km. 950 hadi kufikia Km. 1980 na kiwango kinachobaki ni kiwango cha udongo,”ameongeza.
“Tunaishukuru
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
kutuongezea bajeti mara tatu ya bajeti
ya awali na hivyo tumeweza kuongeza madaraja ya mawe kutoka daraja (1) mwaka
2021 hadi kufikia madaraja (10).”
Pia amesema
wameweza kuongeza madaraja madogo na ya kati kutoka 283 hadi 530 vile vile
madaraja makubwa yameongezeka kutoka madaraja (2) mwaka 2021 hadi kufikia
madaraja (28) kwa mwaka huu wa fedha.
Kwa upande
wa mabadiliko ya tabia nchi na utanzaji wa miundombinu ya barabara, Mhandisi
Bwaya amesema kwamba wanaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara
yanayosababishwa na uharibifu wa miundombinu hasa mifereji, kung’olewa kwa
alama za barabara na uvamizi wa hifadhi za barabara kwa shughuli za kiuchumi
pamoja na umuhimu wa kupanda miti na kutunza mazingira na kuacha kufanya shughuli zingine za
kibinadamu kwenye hifadhi za misitu na kwenye vyanzo vya maji.
Hata hivyo
ametoa wito kwa wananchi kuendelea
kutunza miundombinu ya barabara kwa
kuzingatia sheria na kanuni zake kwani
Serikali inawekeza fedha nyingi kwenye miundombinu ya barabara hivyo ni
wajibu wao kuitunza ili waendelee kunufaika nayo kwa muda mrefu.
Naye, Mkazi
wa Babati Bw. Bakari Sanka amesema Mkoa wao
unapokea mazao mengi kutoka vijijini hivyo kukamilika kwa ujenzi wa
madaraja na miundombinu mingine imewanufaisha wananchi wengi na hivyo shughuli
zao za uzalishaji zinaendelea kama kawaida.
Pia. Bi.
Hadija Shabani amesema wamefurahi sana kwa ujenzi wa madaraja katika kata
zao kwani makorongo yalikuwa mengi na
hivyo msimu wa mvua wanafunzi na watoto walikuwa wakipata shida kuvuka ila kwa
sasa imewaokoa na kuwarahisishia usafiri.
0 Maoni