Julai 07
kila mwaka ni Siku ya Kiswahili duniani, siku iliyopendekezwa na Shirika la
Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) mwaka 2022, ikiwa ni
kuitambua lugha ya Kiswahili kama alama muhimu ya muafrika, yenye wazungumzaji
zaidi ya milioni 350 duniani kote.
Barani
Afrika, lugha ya Kiswahili ni utambulisho wa muafrika, ambapo Mwaka 2019, lugha
ya Kiswahili ilitambuliwa na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC)
kuwa lugha pekee ya Kiafrika.
Baadhi ya
nchi barani Afrika ikiwemo Afrika Kusini, Botswana, Ghana na Ethiopia tayari
zimeanza kufundisha lugha ya Kiswahili Shuleni ikiwa ni jitihada za
kuliunganisha Bara la Afrika, wazo ambalo lilikuwa la baba wa Taifa, Hayati
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika miaka ya 1960.
Serikali ya
Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan imeendeleza maono hayo pamoja na kuja na mikakati kadha wa
kadha ya kukuza lugha hii adhimu, ikiwemo dhana maarufu ya ‘Kuibidhaisha lugha
ya Kiswahili’, dhana inayosisitiza kukuza na kukiuza Kiswahili kama bidhaa nje
ya mipaka ya Tanzania.
Julai 6,
2023 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa
Majaliwa akizungumza katika ufunguzi wa maadhimisho ya siku ya Kiswahili
duniani, aliziagiza wizara zenye dhamana ya lugha ya Kiswahili kusimamia
kikamilifu mkakakti wa kukuza na kubidhaisha lugha ya Kiswahili ndani na nje ya
Tanzania.
“Andaeni
nafasi za Watanzania kufundisha Kiswahili katika nchi mbalimbali duniani, kila
mmoja awajibike kuhakikisha Kiswahilli kinakua na kuendelezwa,” alisema Waziri
Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa.
Pamoja na
mikakati mbalimbali ya kukuza lugha ya Kiswaili, Serikali ya Awamu ya Sita
imeendelea kuweka mazingira mazuri ya kuikuza zaidi lugha ya Kiswahili duniani
ambapo Moja ya mkakati ni kuanzishwa kwa Kongamano la Kimataifa la Kiswahili.
Kongamano
hili ni nyenzo muhimu katika kukuza lugha ya Kiswahili kwa sababu kwa mara ya
kwanza, tangu Tanzania ipate uhuru, Serikali imefanya kongamano la kwanza la
lugha ya Kiswahili jijini Havana, nchini Kuba ikiwa ni hatua ya kwanza ya
kuipeleka lugha hii adhimu ya Kiswahiili duniani.
Akizungumza
katika ufunguzi wa kongamano hilo Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe.
Dkt. Damas Ndumbaro, alifafanua sababu za kufanya kongamano hili nchini Kuba.
“Tanzania ilikuwa kituo muhimu cha wapigania uhuru wa Bara la Afrika, na lugha kuu iliyotumika wakati wa harakati hizo ilikuwa ni Kiswahili. Tunapoendelea na mapambano ya kuleta ukombozi wa kiuchumi katika Bara la Afrika na ambapo tungependa kushirikiana zaidi na wenzetu wa Ukanda wa Karibe, tunaamini Kiswahili kitarahisisha na kuwezesha Mawasiliano kwa ajili ya mtangamano, biashara, utalii na uwekezaji barani Afrika”.
Kadhalika,
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud
Thabit Kombo amewasisitiza watanzania kuchangamkia fursa zilizopo wakati lugha
ya Kiswahili inaendelea kukuwa na kuenea zaidi katika maeneo mbalimbali
duniani.
“Kiswahili
kwa sasa kinazungumzwa na takriban watu milioni 350 na wazungumzaji wanaendelea
kuongezeka. Ni muhimu kuibeba bendera hii vizuri,” alisisitiza Mhe. Balozi
Kombo.
Pamoja na
mambo mengine, uzinduzi wa kongamano hilo la kwanza la kimataifa la Kiswahili
nchini Kuba, umeambatana na uzinduzi rasmi wa Kamusi ya Kihispania kwenda
Kiswahili, Kitabu cha maneno na misemo ya kila siku kati ya Kiswahili na
Kihispania pamoja na uzinduzi wa sanamu ya Baba Taifa, Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere, ikiwa ni ishara ya uhusiano wa kihistoria uliyopo kati ya Tanzania na Kuba
uliyoasisiwa na viongozi wa kwanza wa mataifa hayo, Hayati Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere na Hayati Fidel Castro wa Kuba.
Na. Kelvin
Kanje- Havana, Kuba
0 Maoni