Waziri wa
Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amefanya mazungumzo kwa
njia ya mtandao na ujumbe kutoka Idara ya Uvuvi na Wanyamapori ya Serikali ya
Marekani kujadili pendekezo la Taasisi
Zisizokuwa za Kiserikali la kupinga kuingizwa Marekani nyara zinazotokana na
uwindaji wa tembo katika vitalu vya uwindaji wa kitalii kwenye eneo la West
Kilimanjaro linalopakana na Hifadhi ya Amboseli Nchini Kenya.
Kikao hicho
kimefanyika katika Makao Makuu ya Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania
(TAWIRI) jijini Arusha jana Novemba 14,2024.
Ujumbe wa
Marekani umeeleza kuwa vikundi vilivyopeleka pendekezo (petition) vinadai kuwa
Tanzania inawinda tembo wa amboseli ambao wanafanyiwa utafiti, uwindaji huo
unakiuka makubaliano ya miaka 30 ya kusitisha uwindaji katika eneo la West
kilimanyaro - Amboseli, na unatishia kupotea kwa tembo wenye meno makubwa.
Waziri kwa kushirikiana
na jopo la wataalam wakiongozwa wa Dkt. Alexander Lobora ametoa ufafanuzi kuhusu utaratibu wa uwindaji
wa tembo, mchango wake katika uhifadhi na maendeleo ya jamii na kwamba uwindaji
unafanyika kisheria kwa kuzingatia utafiti na uzoefu wa muda mrefu.
Aidha,
Wizara imekanusha tuhuma hizo na imeushauri uongozi wa US Fish & Wildlife
Service kupuuzia pendekezo lililowasilshwa na vikundi hivyo.
0 Maoni