Benki ya
Maendeleo ya Ujerumani (KFW) kupitia Mradi wa Afue ya UVIKO 19 "Emergency
and Recovery Support for Biodiversity Tanzania (ERB)" ulio chini ya
Shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS), leo tarehe 14 Novemba, 2024,
imekabidhi msaada wa magari mawili (2) aina ya ISUZU FVZ yenye thamani ya zaidi
ya TZS Milioni 600 kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa
ajili ya kusaidia shughuli za uhifadhi katika Pori la Akiba Selous.
Akizungumza
mara baada ya kupokea magari hayo katika
hafla iliyofanyika Ofisi za Makao Makuu ya TAWA Mkoani Morogoro Kamishna wa
Uhifadhi wa TAWA, Mabula Misungwi Nyanda amezishukuru KFW na FZS kwa kazi nzuri
wanazozifanya katika kuimarisha uhifadhi nchini hususani Kwa msaada walioutoa
na kusisitiza kuwa magari hayo ni nyenzo muhimu sana katika kuboresha utendaji
wa TAWA.
"Tunawashukuru
wenzetu wa KFW na FZS pamoja na washirika wengine wa uhifadhi kwa kuendelea
kutuunga mkono katika kuhakikisha tunaimarisha uhifadhi katika maeneo
tunayoyasimamia," amesema Kamishna Mabula.
"Magari
haya yatatumika Kwa kazi nyingi ikiwemo ujenzi wa miundombinu Kwa ajili ya
uhifadhi na utalii, " ameongeza Kamishna Mabula.
Aidha
Kamishna Mabula amewasisitiza Wakuu wa Kanda husika kuhakikisha magari hayo
yanatumika vizuri na kufanyiwa ukarabati kwa wakati ili yaendelee kudumu.
Naye, Meneja
Mradi wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani kwa Bara la Afrika, Bw. Christian
Weidner amesema KFW inajisikia fahari kutoa mchango wao wa uhifadhi katika
mojawapo ya hifadhi kubwa Afrika na kuomba magari hayo yapelekwe Hifadhi ya Selous ili kuweza kuungana na
timu inayoshughulika na miundombinu.
Aidha, amesema Mradi wa Afue ya UVIKO 19 wenye thamani ya EURO Millioni 35 ambao
unatekelezwa kwa ubia Kati ya Shirika la Frankfurt Zoological Society, TAWA na
TANAPA uliletwa nchini Kwa lengo la kusaidia katika shughuli za uhifadhi baada
ya janga la UVIKO 19.
Amesema
kutokana na changamoto ya janga hilo Serikali ya Tanzania ikishirikiana na
Serikali ya Ujerumani walikubaliana kusaidia shughuli za uhifadhi kwenye Pori
la Akiba Selous.
Christian
Weidner amesisitiza kuwa Mradi huo utaendelea kutoa misaada mbalimbali Kwa
ajili ya kusaidia shughuli za uhifadhi katika Pori la Akiba Selous.
"Ziko
rasilimali zingine ambazo zitatolewa na mradi huu ikiwemo matrekta, boti za
doria pamoja na manunuzi ya vifaa mbalimbali Kwa ajili ya kufanikisha
utekelezaji wa shughuli za TAWA kupitia Pori la Akiba Selous," amesema
Christian.
Na. Beatus
Maganja- Morogoro
0 Maoni