Katibu Mkuu
wa Wizara ya Nishati ameongoza kikao cha wadau, na kuhimiza uwekezaji katika
nishati safi na mbadala.
Siku ya
Nishati ya 15.11. 2024 imefanyika kwa mafanikio makubwa katika Banda la
Tanzania mjini Baku, Azerbaijan, ambapo wadau kutoka sekta mbalimbali
walikusanyika kujadili masuala muhimu yanayohusiana na nishati na mazingira.
Katibu Mkuu
wa Wizara ya Nishati, Eng. Felchesmi J. Mramba, alifungua kikao hicho jana
Novemba 15, 2024 na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika
kutatua changamoto za nishati duniani.
Katika kikao
hicho, mada mbalimbali zilijadiliwa, na washiriki walielezea umuhimu wa nishati
safi na nishati mbadala kama njia bora ya kupunguza uharibifu wa misitu
unaosababishwa na utegemezi wa nishati ya mkaa na kuni.
Takwimu
zinaonyesha kwamba takribani asilimia 85.7 ya Watanzania wanategemea mkaa na
kuni kama vyanzo vya nishati, jambo linaloleta athari kubwa kwa mazingira na
misitu ya nchi.
Wadau kutoka
taasisi mbalimbali walizungumza kwa pamoja kuhusu umuhimu wa kuwekeza katika
nishati mbadala.Mhifadhi Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Dkt.
Elikana John, aliwasilisha mada kwa niaba ya TFS, alisisitiza kwamba suluhu za
nishati mbadala kama vile nishati ya jua na upepo zitasaidia kupunguza
utegemezi wa mkaa na kunyanyua hali ya maisha ya wananchi.
Aidha, Naibu
Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Acc. Zainabu Bungwa aliwakumbusha washiriki
umuhimu wa kuwajumuisha vijana katika mikakati ya nishati, akitolea mfano wa
"Dar es Salaam Youth Global Climate Change Declaration of 2023",
mpango uliowezeshwa kwa ushirikiano kati ya TFS na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM). Mpango huu umejizatiti katika kuhamasisha vijana kushiriki katika
uanzishaji wa miradi ya nishati mbadala na kupigania ulinzi wa mazingira.
Naye Katibu
Mkuu wa Ofisi ya Rais, Eng. Cyprian Luhemeja alifunga kikao hicho kwa kutoa
shukrani kwa wadau wote wa ndani na nje ya nchi huku akisisitiza kuwa
ushirikiano kati ya sekta za umma, binafsi, na jamii ni muhimu katika kuvutia
wawekezaji kwa miradi ya nishati.
Aidha
aliwapongeza wadau kwa kujitokeza kwa wingi na kutoa wito kwa sekta mbalimbali
kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha nishati inafika kwa wananchi wote,
ikiwa ni pamoja na maeneo ya vijijini na kwa kila mwananchi mmoja mmoja.
Siku hii ya
Nishati ya Dunia imekuwa ni fursa nzuri kwa Tanzania kuonyesha juhudi zake
katika kukuza nishati safi na mbadala, na pia inatoa mwito kwa wawekezaji
kuwekeza katika miradi ya nishati endelevu, ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya
kiuchumi, kijamii, na kimazingira ya nchi.
0 Maoni