Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Philip Isdor Mpango kuwa mgeni rasmi katika Kongamano la Tatu la Kimataifa la Kisayansi la TAFORI litakalofanyika Desemba 11 hadi 13, 2024 katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha, (AICC) mkoani Arusha.
Haya
yamezungumzwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania
(TAFORI), Dk. Revocatus Mushumbusi wakati akizungumza na waandishi wa Habari
TAFORI Makao Mkuu, Morogoro, Novemba 15, 2024.
Dk.
Mushumbusi amesema kongamano hilo litaongozwa na mada kuu isemayo “ Kurejesha
Mandhari ya Misitu kwa Maendeleo Endelevu na Kukabiliana na Mabadiliko ya
Tabianchi” yaani Restoring Forest Landscapes for Sustainable Development and
Climate Change Mitigation ambapo wadau takribani 400 Kutoka ndani na nje ya
nchi watapata nafasi ya kujadiliana masuala ya Misitu na Nyuki, ikiambatana na
mawasilisho na maonesho ya mazao ya Misitu na Ufugaji Nyuki kutoka kwa wadau.
Wadau hao ni
kama vile, wanasayansi, watunga sera, wanamazingira, watumiaji wa mazao ya
Misitu na Nyuki, wapanda miti, wafugaji wa Nyuki, Taasisi za utafiti, vyuo
vikuu, Taasisi za Kiserikali na zisizo za Kiserikali na wanafunzi.
Aidha,
Mkurugenzi Mkuu wa TAFORI Dkt. Mushumbusi amesema lengo la kongamano hilo ni;
Moja,
kuwakutanisha wataalamu wa Misitu na ufugaji Nyuki, kujadiliana kwa pamoja na
kubadilishana uzoefu juu ya usimamizi wa maliasili hasa Misitu na ufugaji
Nyuki.
Mbili,
Kupitia kongamano hili, wataalamu wa ndani na nje ya nchi wataweza kutumia
nafasi hii kutoa matokeo ya tafiti zilizofanyika.
Tatu, kuibua
miradi mipya ya uhifadhi kwa lengo la kurejesha na kuongoa Misitu kwa maendeleo
endelevu na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Nne, Kuunga
mkono jitihada za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania alizozifanya za kutangaza vivutio vya utalii kupitia filamu ya
‘‘Tanzania The Royal Tour na Amazing Tanzania.”
Vilevile,
Kongamano hili litakuwa ni sehemu ya kuchochea na kuhamasisha wadau mbalimbali
kushirikiana na Serikali kwenye maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Wafugaji Nyuki Duniani
(APIMONDIA) utakaofanyika nchini mwaka 2027.
Hata hivyo,
Mkurugenzi Mkuu wa TAFORI Dk. Mushumbusi amewasihi wadau kushiriki katika
Kongamano hilo kwani kushiriki kwao ni sehemu ya majukumu ya Taasisi katika
kuhakikisha inasambaza matokeo ya tafiti za Misitu na ufugaji Nyuki kwa
watumiaji wa mwisho nchini Tanzania na kutoa majibu ya changamoto zinazoikabili
sekta hiyo.
0 Maoni