Hifadhi ya Taifa Arusha yapongezwa utekelezaji maelekezo ya Mawaziri

 

Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Musa Nassoro Kuji ameipongeza Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Arusha kwa hatua inazochukuwa katika utekelezaji wa maelekezo ya mawaziri nane kuhusu utatuzi wa migogoro ya mipaka baina ya hifadhi na maeneo yanayoizunguka hifadhi hiyo.

Kamishna Kuji, ameyasema hayo katika ziara yake ya kikazi aliyoifanya jana tarehe 15, Novemba 2024 katika hifadhi hiyo ikiwa na lengo la kuzungumza na Menejimenti ya hifadhi, Maafisa pamoja na Askari wa Uhifadhi waliopo katika hifadhi hiyo.

“Kila hifadhi iwe bunifu kutatua migogoro kwani palipo na amani kuna maendeleo. Nitumie fursa hii kuipongeza Menejimenti ya hifadhi kwa kazi nzuri ya kutatua changamoto za mipaka kwani ndio maelekezo ya Wizara na Serikali.”

“Nimepokea mawazo na michango mizuri yenye kujenga Shirika letu kutoka kwa Menejimenti, Maafisa na Askari wa Uhifadhi hivyo natambua na kuthamini mawazo na michango ya kila mmoja katika kuleta maendeleo ya Shirika na Taifa kwa ujumla na nisisitize bidii na weledi katika kutekeleza majukumu yetu.”

Akiwasilisha taarifa ya hifadhi, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Eva Malya ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Arusha alimpongeza Kamishna Kuji kwa kutenga muda wake na kwenda kuitembelea hifadhi, kusikiliza changamoto pamoja na kuzungumza na Maafisa na Askari wa Jeshi la Uhifadhi waliopo katika hifadhi hiyo. Kamishna Malya aliongeza kuwa uongozi wa Shirika kwa kushirikiana na Menejimenti ya hifadhi unatarajia kulipa fidia kaya 51 katika kitongoji cha Nasula ili kupisha shughuli za uhifadhi na utalii.

“Ninaishukuru Bodi ya Wadhamini, pamoja na Menejimenti ya Shirika kwa mchango na maelekezo wanayotupatia katika kufanikisha utatuzi wa migogoro. Pia, kwako Afande Kamishna kwa kupanga na kuifanya ziara hii ya kutembelea Hifadhi ya Taifa Arusha, kukutana na kuzungumza na sisi. Kwaniaba ya Maafisa na Askari Uhifadhi tunakuahidi kuendelea kutekeleza majukumu yetu kwa ari kubwa na kuzingatia miongozo ya Shirika na vipaumbele vya Taifa katika sekta ya utalii na uhifadh,” alisema Kamishna Malya.

Mapema jana, Mhe.Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb), Waziri wa Maliasili na Utalii katika ziara yake ya kikazi Makao Makuu ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), alitoa maelekezo mahususi kwa taasisi zote zilizopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuendelea kuzingatia maelekezo yote yaliyotolewa na timu ya mawaziri nane katika utatuzi wa migogoro ya mipaka.

Na. Edmund Salaho- Arusha

Chapisha Maoni

0 Maoni