Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Serikali imeendelea kutekeleza miradi
mingi katika sekta ya afya inayolenga kuongeza ufanisi katika huduma za afya na
kuboresha maisha ya Watanzania.
Sambamba na kulipongeza Kanisa
Katoliki kwa juhudi zake za kutoa huduma za afya katika maeneo mbalimbali
wakati ambao Serikali pia imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya
afya.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Novemba
1, 2024 Sengerema mkoani Geita wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uzinduzi wa jengo la jipya la
kisasa la upasuaji na mradi wa umeme wa jua katika hospitali ya Sengerema DDH
iliyopo chini ya Kanisa Katoliki, Jimbo Katoliki la Geita.
Akitaja baadhi ya mafanikio ya
Serikali katika sekta hiyo Dkt. Biteko amesema
“ Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais
Samia imefanya kazi nyingi ikiwemo kujenga hospitali mpya 129, kukarabati
hospitali kongwe 50, kujenga hospitali za wilaya 677 na zahanati 425. Nawaomba
watu Sengerema na sisi wote kwa kujua wafadhili wametoa fedha kwa ajili ya
ujenzi wa jengo hili na mradi wa umeme wa jua wamejinyima kwa ajili yetu hivyo
tutunze miundombinu hii,”
Amesisitiza “Tutatibiwa sisi kutoka
Kigoma na Kagera na wakati wa Covid 19 hapa palikuwa na msaada mkubwa haitakuwa
sawa wakati mwingine wakija wakakuta tumepabadilisha na kuwa tofauti na lengo
lao, tutunze vifaa hivi na majengo haya na tuwape moyo ili waweze kutusaidia
katika maeneo mengine yenye uhitaji,”
Ameendelea kwa kuwashukuru wafadhili
wa miradi hiyo na kuifanya hospitali hiyo kuwa bora na ya kisasa.“
Tunasheherekea mafanikio haya kwa sababu
umisionari umelenga kuhudumia watu kiroho na kimwili, niwapongeze sana Kanisa
Katoliki kwa kuunga mkono juhudi ambazo Serikali ingefanya, pamoja na kuhubiri
watu kutenda mema na kuponya magonjwa yao na kuwaondoa kwenye umasikini hilo ni
jambo muhimu,”
Aidha, Dkt. Biteko amebainisha kuwa
Serikali inathamini mchango wa kanisa katika maendeleo ya watu.
Akizungumzia Dira ya Maendeleo ya
Taifa ya Mwaka 2050, amesema inajengwa kwa msingi wa amani na usalama huku
akiwaomba viongozi wa dini kuendelea kuhubiri amani na kuwaweka pamoja
Watanzania ili waendelee kujenga nchi yao.
Fauka ya hayo, Dkt. Biteko amewaasa
Watanzania kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa amani na kufuata
taratibu na sheria na kuwa uchaguzi huo usiwe sababu ya kuwagawa.
Naye, Mbunge wa Sengerema, Mhe. Hamis
Mwagawa amemshukuru mtawa Dkt. Marie Jose na kumpongeza kwa kutoa huduma kwa
wananchi na kusema kuwa hata wakati wa janga la Covid 19 pamoja na
kuwashukuru wafadhili wote waliojitolewa
kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo la upasuaji.
Kwa upande wake Askofu wa Jimbo
Katoliki Geita, Flavian Kassala amesema ujenzi wa hospitali hiyo ulianza kutoka
na ujio wa watawa sita na familia moja waliohitaji kujenga hospitali ambayo
ingetoa huduma ya afya kwa wahitaji na baadaye hospitali hiyo ikawa teule hadi
mwaka huu ambapo Serikali imejenga hospitali yake ya wilaya.
“Tuna juhudi katika kuendesha huduma
kwa gharama nafuu na tuna mfuko wa kusaidia wahitaji ambapo tunapata misaada
kutoka Shirika la Marafiki wa Sengerema na Simba Health ambao walikuja na wazo
la kuwa na chumba cha upasuaji chenye vifaa vya kisasa na sasa tumepata jengo
hili ambalo litasaidia kutoa huduma za kisasa za upasuaji,” amesema Askofu Kassala.
Ameendelea kusema baada ya kuwa na
jengo hilo lilikuja wazo kutoka Shirika la Marafiki wa Sengerema ambao ni
madaktari wanafunzi kutoka Uholanzi la kupendekeza mradi wa umeme mkubwa wa jua
ili pia usaidie kutumika katika mifumo ya CT scan na MRI.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Sengerema
Sr. Dkt. Marie Jose amesema kuwa hospitali hiyo ina uwezo wa kulaza wagonjwa
22,000 na inatoa huduma za kibingwa kwa akina mama na watoto pamoja na kuwa
sehemu ya kufanya mafunzo kwa vitendo
kwa madaktari wanafunzi kutoka Hospitali ya Kanda ya Bugando.
“Tumeanza kuboresha huduma zetu na
idara ya mionzi ina mitambo mipya, tuna huduma ya watoto wanahohitaji huduma
maalum na tuna umeme wa jua ambao ni wa
uhakika. Leo ni siku ya furaha tuna jengo hili ambalo limegharimu shilingi
bilioni 2.7 na mradi wa umeme wa jua umegharimu shilingi bilioni 1.7,” amesema Dkt. Jose.
Moja ya mfadhili wa jengo la upasuaji,
Bibi. Doris Mars amesema kuwa walipopata wazo la ufadhili wa mradi huo yeye na
familia yake waliamua kusaidia kwa kuwa mradi huo unalenga kuboresha maisha ya
watu.
“Mungu ametupa uwezo wa kusaidia
wengine na Biblia Takatifu inatuambia kila binadamu ameumbwa kwa sura na mfano
wake hivyo tunaamini tutasaidia kuokoa maisha na kuwapa faraja watu wa
Sengerema pia tunawashukuru wote walioto mchango wao katika miradi hii,”
amesema Bibi. Mars.
Mwakilishi wa Sopowerful, Dkt. Koen
Gelpke amesema kuwa uwepo wa jengo la kisasa ulihitaji pia umeme wa uhakikia ili
kutoa huduma kwa wananchi na ndio sababu waliamua kujenga mradi wa umeme wa
jua.
Awali Dkt. Biteko ameshiriki katika
adhimisho la Misa Takatifu kwa ajili ya ufunguzi wa jengo jipya la kisasa la
upasuaji.
Akihubiri katika misa hiyo , Mhashamu Askofu Mkuu wa Jimbo la Songea, Damiani Denis Dalu
amesema kuwa siku ya leo ni sikukuu ya
watakatifu wote na ni sherehe kubwa katika liturijia na kuwa wanawakumbuka watakatifu wote.
Amefafanua kuwa watakatifu hao ndio
waliofaulu na kuwekwa wafu ili kuwa kuelelezo cha watu wote kuwa maisha ya kumfuata yesu kristo yana
tija mbinguni.
Askofu Dalu ameendelea kusema kuwa
Kanisa Katoliki ni la kimisionari ambapo walitumwa mitume 12 dunia kote kwa
ajili ya kuhubiri injili.
“Wamisionari wa Afrika ndio
waliohubiri injili eneo hili katika uinjilishaji wao walihakikisha kila
wanapifika wanatoa huduma za afya, elimu na za kijamii kwa ujumla. Na hii ni
Parokia ya Bikira Maria Afya ya Wagonjwa eneo hili wamisionari walifungua kituo
cha wagonjwa na waliwajengea pia eneo kwa ajili ya kusali,” amesema Askofu Dalu.
Amesisitiza “Tunamshukuru Mwasisi wa
Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kuenzi na kutambua huduma hizi kwa
watu na Serikali kwa kuendeleza hili. Leo tunamshukuru Mungu na tuzidi
kuombeana ili hiki tunachoenda nacho kikae sawa, tunashukuru kwa juhudi ambazo
Serikali imezifanyq katika hospitali hii mwaka
2013 hadi 2015.”
Pia, Askofu Mkuu Dalu amewashukuru
wafadhili kutoka nchini uholanzi kwa mchango wao katika hospitali ya Sengerema
DDH “ Tunakoeleka ni kuzuri na tunawashukuru sana wafadhili wetu kwa uinjilishaji huu, tunamshukuru pia Askofu kwa
urafiki kati ya dayosisi hizi na kutusaidia katika Sengerema Hospitali na kituo
cha mafunzo.”
0 Maoni