Rais Samia Suluhu Hassan amewahakikishia Watanzania kuwa serikali itagharamia matibabu ya majeruhi na kuwasitiri waliofariki katika tukio la kusikitisha la kuporomoka kwa jengo la ghorofa Kariakoo, jijini Dar es Salaam.
Rais Samia amethibitisha
kuwa watu 13 wamepoteza maisha katika ajali ya jengo hilo lenye maduka lililoporomoka
jana majira ya asubuhi.
Rais Samia ametumia
fursa hiyo kutoa pole kwa ndugu, jamaa, na marafiki wa waathirika wa tukio
hilo, na kuwaomba Watanzania wote kuwaweka kwenye maombi wale wote
walioathirika na kuwaombea pumziko la amani waliopoteza maisha.
"Mpaka
sasa, sababu za kitaalamu za kuporomoka kwa jengo hilo bado hazijachunguzwa na
kubainishwa kwani kipaumbele chetu kwanza kilikuwa ni kuwaokoa wenzetu waliokuwamo
kwenye jengo hilo," alisema Rais Samia.
Aidha, Rais
Dkt. Samia amesema baada ya zoezi la uokoaji kukamilika, anamtaka Waziri Mkuu
Mhe. Kassim Majaliwa aongoze timu ya wakaguzi majengo ili wakague eneo lote la
Kariakoo na kutoa ripoti kamili ya hali ya majengo katika eneo hilo.
Kwa upande
wa Jeshi la Polisi, Rais Samia amelitaka lipate taarifa kamili kwa mmiliki wa
jengo lililoporomoka jinsi ya ujenzi ulivyokuwa.
Pamoja na
mambo mengine, Rais Samia alisisitiza kuwa serikali imejitolea kuokoa na
kuwasaidia waathirika wa tukio hili kwa kila hali, huku akitoa wito kwa
wananchi kuendelea kuwa na subira na kuungana katika kipindi hiki kigumu.
0 Maoni