Mfumo wa
Usimamizi wa Ununuzi wa Umma Kielektroniki (NeST) umeshinda tuzo ya “Mfumo Bora
wa Ununuzi wa Umma Barani Afrika” katika tuzo za African Association for Public
Administration and Management (AAPAM), zilizokuwa zikishindaniwa chini ya
uangalizi wa Umoja wa Afrika (AU), jijini Kampala, Uganda.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Kampala, baada ya kupokea tuzo hiyo mbele ya
mamia ya washiriki wa Mkutano wa AAPAM, Novemba 28, 2024, Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), inayosimamia NeST, Bw. Dennis
Simba, alisema kuwa tuzo hii ni heshima kubwa kwa Tanzania, kwani ununuzi wa
umma ni moja ya maeneo yanayotumia asilimia kubwa ya fedha za umma barani
Afrika.
"Tuzo
hii imetuletea heshima kubwa, kwani tulifika katika tano bora kati ya washiriki
69 na ni sisi pekee ambao tumeingiza mfumo wa ununuzi wa umma na leo
umetambulika na kupewa tuzo hii…ni mafanikio makubwa kwa Tanzania na kwa mfumo
wetu," alisema Bw. Simba na kuelekeza pongezi za kipekee kwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyewezesha kuanzishwa
kwa sheria ya ununuzi wa umma ya Mwaka 2023, na kuundwa kwa NeST, mfumo ambao umetambulika
Afrika nzima kwamba ni bora wa ununuzi wa umma."
Bw. Simba
alisema kwa kuwa mfumo huu umejengwa na wataalam wa Tanzania pekee, PPRA iko
tayari kushirikiana na nchi nyingine kuhakikisha kuwa teknolojia hii inawafikia
na kusaidia katika mageuzi ya sekta ya ununuzi wa umma barani Afrika.
Ameishukuru
Wizara ya Fedha kwa kuwazesha ujenzi wa Mfumo wa NeST na ufuatiliaji wake wa
karibu kila hatua kuhakikisha maono ya Mheshimiwa Rais yanatekelezwa kwa
vitendo.
Aidha,
alisema kuwa ujenzi wa Mfumo huu umewezekena kwa kutumia kwa ushirikiano kati
ya PPRA na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) ambao walitoa wataalam na
miongozo.
Kwa upande
mwingine, mfumo wa kutoa huduma ya afya kwa jamii nchini Kenya umeshinda tuzo
ya jumla, huku Uganda ikikabidhiwa Tuzo Maalum (Special Award) kwa kuwa
mwenyeji wa mkutano wa AAPAM.
0 Maoni