Mtendaji
Mkuu wa Wakala ya Barabara ya Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Victor Seff
leo tarehe 19 Novemba, 2024 amekutana na kufanya kikao na Mameneja wa Mikoa
kwenye Ofisi za Makao Makuu za Wakala hiyo zilizopo Mji wa Serikali
Mtumba,  jijini Dodoma.
Katika kikao
hicho Mhandisi Seff amewataka Mameneja hao kwenda kuwasimamia Mameneja wa
Wilaya katika maeneo yao na kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu wakati wote
wanapotekeleza majukumu yao.
Amesema
Mameneja hao wanapaswa kulinda taaluma zao pale wanapotekeleza majukumu yao ya
kila siku ili kulinda sifa nzuri ya Wakala.
Aidha,
Mhandisi Seff amewataka Mameneja hao kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye
miradi wanayoitekeleza katika Wilaya zao.
“Nimepita
kwenye baadhi ya Mikoa na Wilaya, nimeona kuna barabara ambazo hazifanyiwi
matengenezo. Pia yapo madaraja ambayo hayasafishwi na hivyo kuweza kuleta
madhara wakati wa msimu wa mvua.”
Hivyo
amewataka Mameneja hao kwenda kusimamia na kuhakikisha wanafanya matengenezo ya
barabara kama inavyotakiwa pia kusafisha madaraja ili kutokuleta mafuriko
wakati wa msimu wa mvua unaokaribia.
Naye,
Mkurugenzi wa Huduma Saidizi Bi. Azimina Mbilinyi amewataka Mameneja hao
kuwasimamia vyema watumishi walio chini yao kwenye utunzaji wa vifaa vya kazi,
utunzaji wa siri pamoja na kushirikiana na taasisi nyingine zinazowazunguka
kwenye Mikoa yao.


0 Maoni