Katibu wa
NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM, CPA Amos Makalla, ameitaka Ofisi ya Rais
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kutenda haki kwa vyama vyote
vilivyosimamisha wagombea katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na
vitongoji.
Amesema
katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu, wapo wagombea
wa CCM ambao wamewekewa pingamizi, hivyo madai ya vyama vya upinzani kwamba
wagombea wao pekee ndiyo waliowekewa pingamizi yanalengo la kuwahadaa
Watanzania.
Makalla
ameyasema hayo leo wakati akizungumza na viongozi na wanachama wa CCM Wilaya ya
Temeke jijini Dar es Salaam, ambapo amesisitiza kuwa CCM ipo tayari kushiriki
uchaguzi huo na itaibuka mshindi kwani imejiandaa ipasavyo.
“Nitume
nafasi hii kuwaomba TAMISEMI ambao ndiyo wasimamizi wa uchaguzi huu, waitendee
haki CCM na vyama vingine vyote vitendewe haki. Tunaamini uchaguzi utakuwa huru
na haki na atakayeshinda kwa haki, atangazwe.
Amesema
kwamba CCM haihitaji upendeleo, haihitaji kubebwa, kwa kuwa ipo tayari kwani walishajipanga
kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Taarifa
zinasema kuwa jumla ya wagombea Tisa wa Chama Cha Mapinduzi kwenye Halmashauri
ya Jiji la Arusha Mkoani Arusha wameenguliwa kwenye mchakato wa Uchaguzi wa
serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024 kutokana na kutokidhi
matakwa ya kikanuni na sheria za uchaguzi huo.
Kulingana na
Msimamizi wa Uchaguzi, Wagombea hao wamekosa sifa kutokana na sababu mbalimbali
ikiwemo mitaa wanayogombea kutokuwepo kwenye orodha ya mitaa inayotambulika na
Mamlaka ya serikali za mitaa pamoja na kutoainisha Jinsia zao kwenye fomu
walizozijaza.
Miongoni mwa
walioenguliwa ni pamoja na Frank Samwel Laizer aliyekuwa anagombea uenyekiti wa
Mtaa wa Mbeshere, David Molel aliyekuwa anawania uenyekiti Mtaa wa Olkungu na
Mohamed Amir aliyekuwa anawania Uenyekiti wa Mtaa wa Makaburi ya Baniani pamoja
na Juma Waziri aliyekuwa mgombea Uenyekiti serikali ya mtaa wa Mkwangwaru B.
Aidha, pia
wamo wagombea wa Ujumbe wa serikali za mitaa akiwemo Hayrat Manyanga na Gilbert
Massawe ambao pia wameshindwa kuendelea na uchaguzi huo wa baadae mwezi huu
kutokana na dosari mbalimbali katika ujazaji wa fomu za
kuwania nafasi hizo.
0 Maoni